Viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali nchini wamekumbushwa kuimarisha mahusiano kati ya taasisi za dini na Serikali ili kudumisha amani, umoja na mshikamano, huku akiwataka vijana kutumia fursa zilizopo nchini kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Ujumbe huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipokuwa akizungumza na waumini wa Kanisa la Shekina jijini Dar es Salaam. Amesema ushirikiano mzuri kati ya taasisi za dini na Serikali ni nguzo muhimu ya kudumisha utulivu wa nchi.
Sangu ameeleza kuwa taasisi za dini zina nafasi kubwa katika kujenga maadili ya jamii na kusaidia juhudi za Serikali katika kuhakikisha amani na mshikamano vinaendelea kuimarika nchini.
Aidha, amewahimiza vijana kuachana na tabia ya kukaa vijiweni bila kufanya kazi, akisisitiza kuwa kuna fursa nyingi za kiuchumi zinazoweza kuwasaidia kujitegemea iwapo watazitumia ipasavyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CPCT Mkoa wa Dar es Salaam, Mika Fonka, amesema kanisa lipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kudumu, huku akihimiza ushirikiano huo kupewa kipaumbele.
Baadhi ya waumini waliohudhuria ibada hiyo wamesema ni wakati muafaka wa kuimarisha uhusiano kati ya dini na Serikali ili kulinda umoja wa kitaifa, wakisisitiza kuwa mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.

0 Maoni