Pasaka yahitimishwa kwa wito wa amani na haki taifa zima

Sherehe za Pasaka zinazoadhimisha ufufuko wa Mwokozi Yesu Kristo zimehitimishwa jana nchini, huku kukiwa na msisitizo mkubwa kutoka kwa viongozi wa dini na serikali kuhusu umuhimu wa kuendeleza maisha yanayoakisi huruma, upendo, msamaha na amani.

Viongozi hao wamehimiza kuwa maadili yaliyopatikana katika kipindi cha Kwaresma na Pasaka hayapaswi kuishia na msimu huo, bali yanatakiwa kuwa muundo wa maisha ya kila siku ya Mtanzania ili kudumisha utulivu wa taifa.

Rais Samia Suluhu Hassan, katika salamu zake kwa Watanzania, amesisitiza kuwa mshikamano wa kitaifa ndio nguzo muhimu itakayolifikisha taifa katika hatua za juu za maendeleo.

Rais alihimiza wananchi kuyaenzi mafundisho ya Kristo kwa vitendo, hususan katika kuwajali wengine na kudumisha umoja, akibainisha kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kujenga jamii yenye maendeleo endelevu ya kiroho na kimwili.

Aliongeza kuwa Watanzania wana wajibu wa kuilinda amani ya nchi kwa wivu mkubwa ili kuruhusu shughuli za maendeleo kuendelea.

Nao viongozi wa dini, wakiwemo Askofu Jackson Sosthenes wa Anglikana, Askofu Dk. Alex Malasusa wa KKKT, na Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, walitumia mahubiri yao kuitaka jamii kutatua tofauti zao kwa amani.

Walieleza kuwa Pasaka ni fursa ya kutafakari upya uhusiano wa kijamii na kuimarisha utu na kuheshimiana, jambo ambalo litaifanya Tanzania kuendelea kuwa mahali salama na pazuri pa kuishi kwa kila mmoja.

Kwa upande wake, Paroko wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Chrisant Mganga, ameweka msisitizo wa kipekee katika suala la haki. Akihutubia waumini katika mkesha wa Pasaka jijini Dodoma, Paroko Mganga alisema kuwa haki ni nguso inayowafanya watu kuishi kwa umoja na kuridhika na nafasi zao katika jamii. Alibainisha kuwa pale ambapo haki inatawala katika maamuzi na matendo, amani huchanua na mshikamano huimarika miongoni mwa wananchi bila kulazimishwa.

Paroko Mganga alihitimisha kwa kuwahimiza waumini kuwa "watu wapya" katika familia na sehemu zao za kazi kwa kuendeleza matendo ya huruma yaliyopamba kipindi cha Kwaresma. Alisisitiza kuwa mabadiliko ya kweli yanatokea pale kila mmoja anapojitahidi kutenda mema na kutoa elimu kwa uvumilivu kwa wengine ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

Wito huu wa pamoja wa viongozi wa kiroho na kiserikali unatoa mwelekeo wa namna Tanzania inavyoweza kuendelea kuwa kisiwa cha amani kupitia mabadiliko ya tabia ya mtu mmoja mmoja.

Chapisha Maoni

0 Maoni