Mradi wa umwagiliaji Makambako kuinua uchumi wa wakulima

Serikali imetangaza kuanza kwa mradi mkubwa wa umwagiliaji katika eneo la Idofi, Wilaya ya Makambako, hatua inayolenga kukuza uchumi wa wananchi kupitia kilimo cha tija.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Idofi, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa bwawa la kisasa na mifumo ya usambazaji maji itakayotosheleza ekari 1,300.

Utekelezaji wa mradi huu ni kielelezo cha jinsi amani na utulivu wa nchi unavyotoa nafasi kwa serikali kuelekeza nguvu katika miradi ya kimkakati ya kuwaendeleza wananchi wake kiuchumi.

Waziri Chongolo alibainisha kuwa kwa sasa ni chini ya ekari 300 pekee ndizo zinazolimwa kutokana na uhaba wa maji na miundombinu duni, hivyo uwekezaji huo unaofanywa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji utaleta mageuzi makubwa kwa kuruhusu kilimo cha mwaka mzima.

Katika kutoa hofu kwa wakazi wa eneo hilo, Waziri alisisitiza kuwa hakuna mkulima atakayepoteza umiliki wa ardhi yake kutokana na mradi huo. Alieleza kuwa wananchi wataendelea kumiliki maeneo yao, lakini aliwataka kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuruhusu ujenzi kukamilika kwa haraka kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya kilimo kama injini ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Makambako, Kenneth Haule, aliwahimiza wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa kujifunza kutoka katika maeneo mengine kama Igomelo na Pawaga, ambako miradi kama hiyo imeweza kuongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa. Alisema kuwa mradi huo ni fursa ya dhahabu kwa wakulima wa Makambako kujikwamua na umaskini kupitia kilimo cha biashara.

Viongozi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wamethibitisha kuwa ushirikishwaji wa wananchi ndio kipaumbele chao kikuu katika kila hatua ya usanifu na ujenzi.

Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Njombe, Machage Mwema, alihitimisha kwa kuwahakikishia wananchi kuwa utaratibu wa kisheria wa umiliki wa ardhi utazingatiwa, huku lengo kuu likibaki kuwa ni kuboresha miundombinu ili kuongeza thamani ya ardhi yao na kipato cha kaya.

Chapisha Maoni

0 Maoni