Mama Lishe Feri Wasisitiza Utu na Upendo Kudumisha Amani

Wafanyabiashara wa vyakula maarufu kama mama lishe katika eneo la Soko la Kimataifa la Samaki la Feri jijini Dar es Salaam wameeleza kuwa utu, upendo na uvumilivu ni msingi muhimu wa kudumisha amani na utulivu katika jamii.

Akizungumza katika eneo lake la biashara, Halima Manjoti amesema kuwa katika shughuli zao za kila siku hukutana na watu wa makundi na mitazamo tofauti, hivyo ni lazima kuwa na moyo wa kuvumiliana ili kuendelea kuishi kwa amani na kuwahudumia wateja wao ipasavyo.

Kwa upande wake, Mary Mgawe amebainisha kuwa upendo miongoni mwa Watanzania husaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima, akieleza kuwa pale watu wanapojali na kuheshimiana, jamii huwa imara na yenye mshikamano.

Naye Sikitu Saleh amesema kuwa utu ni tunu muhimu inayopaswa kuendelezwa, hasa kwa vijana, akisisitiza kuwa maadili mema yana mchango mkubwa katika kulinda amani ya nchi na kuimarisha mahusiano ya kijamii.

Aidha, mama hao wameeleza kuwa biashara zao zinanufaika zaidi pale kunapokuwa na utulivu, kwani wateja huweza kufika kwa uhuru bila hofu, hali inayochangia ukuaji wa kipato chao na uchumi kwa ujumla.

Kwa pamoja, wametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuenzi misingi ya utu, upendo na kuvumiliana, wakisisitiza kuwa kudumisha amani na utulivu ni jukumu la kila mmoja kwa maendeleo endelevu ya taifa.

#SisiNiWamoja

Chapisha Maoni

0 Maoni