Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimefungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, hatua inayolenga kuimarisha biashara ya kikanda na kuongeza uwekezaji baina ya mataifa haya mawili.
Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, alisisitiza
kuwa TanTrade ni daraja la biashara kati ya Tanzania na mataifa ya
nje, akiwakaribisha wafanyabiashara kutoka DRC kutumia fursa zilizopo
nchini. Alieleza kuwa Tanzania imejipanga kutumia lango la magharibi
kupitia Kigoma katika kuimarisha biashara kwenye nchi za Ushoroba wa
Kati kwa kurahisisha huduma za usafirishaji na upatikanaji wa bidhaa
za viwandani na vyakula ili kuongeza mchango wa sekta binafsi katika
uchumi wa kikanda.
Kwa upande wake, Gavana wa Jimbo la Kivu
Kusini (Bukavu), Profesa Jean-Jacques Purusi Sadiki, amewahimiza
wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza nchini DRC, akibainisha kuwa
kuna nafasi nyingi za kibiashara na uwekezaji katika sekta
mbalimbali. Aliongeza kuwa serikali ya DRC itaendelea kuhakikisha
mazingira salama kwa wawekezaji, ili kuimarisha uhusiano wa kiuchumi
na kukuza biashara ya kikanda.
Aidha, Gavana ameishukuru
TanTrade kwa mwaliko wa kuja kushiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya
Kimataifa SabaSaba na amesema ataambatana na wafanyabiashara wakubwa
ili kupata fursa zaidi za biashara katika maonesho hayo yatakayoanza
tarehe 28 Juni 2026.

0 Maoni