Bunge
la Jamhuru ya Muungano wa Tanzania, limeridhia na kupitisha bajeti ya
Wizara ya Madini ya shilingi bilioni 174.9 kwa Mwaka wa Fedha
2026/2027 ili kuiwezesha Wizara ya Madini kufanikisha ukusanyaji wa
maduhuli ya shilingi trilioni 1.4.
Akiwasilisha Bungeni
makadirio ya Mapato na Matumizi leo Aprili 27, 2026, Waziri wa
Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema fedha hizo zitawezesha
kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na taasisi
zilizo chini yake, huku zikilenga kuendeleza kasi ya ukuaji wa sekta
ya madini kwa kufanya tafiti za jiosayansi nchini.
Akifafanua
mgawanyo wa Bajeti hiyo, Waziri Mavunde amesema kiasi cha shilingi
bilioni 71.5 sawa na asilimia 40.9 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya
maendeleo, wakati shilingi bilioni 103.5 sawa na asilimia 59.1 zikiwa
ni matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 27.4 ni
mishahara ya watumishi na shilingi bilioni 76.1 ni matumizi mengineyo
ya Wizara na taasisi zake.
Kuhusu mwenendo wa Sekta, Waziri
Mavunde amefanunua kuwa, mchango wa Sekta ya Madini katika kuchangia
katika Pato la Taifa umeendelea kuimarika, ukiongezeka kutoka
asilimia 9.1 mwaka 2023 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024, na kufikia
wastani wa asilimia 11.9 mwaka 2025.
Aidha, Waziri Mavunde
ameongeza kuwa ukusanyaji wa maduhuli umeongezeka kwa kiwango
kikubwa, kutoka shilingi bilioni 753.2 mwaka 2023/2024 hadi shilingi
trilioni 1.07 mwaka 2024/2025. Kwa kipindi cha miezi tisa ya mwaka
2025/2026 (Julai hadi Machi), tayari shilingi trilioni 1.03 sawa na
asilimia 114.9 ya lengo lililopangwa.
Katika kuimarisha
biashara ya madini, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, idadi ya masoko
imeongezeka kutoka 43 hadi 44, huku vituo vya ununuzi vikiongezeka
kutoka 114 hadi 118, hatua inayolenga kuongeza uwazi na ushindani wa
bei kwa wachimbaji.
Ametaja vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka wa
Fedha 2026/2027 kuwa ni kuimarisha mchango wa sekta katika uchumi,
kuendeleza mnyororo wa thamani madini muhimu na ya kimkakati, pamoja
na kuhamasisha uwekezaji katika uongezaji thamani.
Vipaumbele
vingine ni kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya
vito, kuongeza uwekezaji katika tafiti za kina za madini, kurasimisha
na kuwaendeleza wachimbaji wadogo, ikiwa pamoja na kuzijengea uwezo
taasisi zilizo chini ya Wizara ili kuongeza tija na ufanisi.
Kwa
upande wake , Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa amesema kuwa
, Wizara ya Madini itaendelea kuimarisha ukaguzi katika migodi midogo
na mikubwa ili kuongeza ufanisi katika uzalisha madini.
Akielezea
kuhusu mageuzi ya utoaji leseni Dkt.Kiruswa amesema kuwa Wizara ipo
mbioni kuweka mifumo ya utoaji leseni kidigitali jambo litakalo
rahisisha utoaji leseni bila mgongano wa kimaslahi.


0 Maoni