TRILIONI 4.2 MTWARA: Rais Samia anasa "Wabobevu" wa chuma duniani kutoka Italia

Diplomasia ya uchumi ya Tanzania imeendelea kuchanja mbuga kwa kishindo baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Machi 29  kufanya mazungumzo ya kimkakati na Balozi wa Italia, Giuseppe Sean Coppola, aliyeambatana na vigogo wa Danieli Group ambao ni vinara wa teknolojia ya chuma duniani.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es salaam  ujumbe huo kutoka Italia umewasilisha nia thabiti ya kuwekeza takribani Euro bilioni 1.5, sawa na Shilingi trilioni 4.2 za Kitanzania, kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kisasa na kikubwa cha chuma mkoani Mtwara.

Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano na mwekezaji mzawa, hatua inayolenga kugeuza ukanda wa Kusini kuwa kitovu kipya cha viwanda vizito barani Afrika.

Rais Samia amekaribisha nia hiyo kwa mikono miwili, akisisitiza kuwa Tanzania sasa ni kituo shindani na cha kuaminika kwa uwekezaji wa kimkakati kutokana na rasilimali zake asilia na mazingira bora ya biashara yanayozidi kuimarika.

Alibainisha kuwa serikali yake inatafuta washirika wanaoleta teknolojia inayoongeza thamani ya rasilimali za ndani, kuzalisha ajira kwa vijana, na kusaidia dira ya muda mrefu ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2050.

Uwekezaji huu wa Danieli Group unakuja kama matokeo ya Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, ukidhirisha kuwa majadiliano ya kidiplomasia sasa yanatafsiriwa kuwa miradi mikubwa inayoshikika.

Kwa upande wake, Balozi wa Italia ameeleza kuwa ujio wa Danieli Group ni sehemu ya utekelezaji wa "Mpango wa Mattei kwa Afrika," unaolenga kukuza ushirikiano endelevu wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Mtendaji Mkuu wa Danieli Group, Giacomo Mareschi Danieli, amekiri kuvutiwa na Tanzania kutokana na uwepo wa nishati ya gesi asilia, madini ya chuma, na nafasi ya kijiografia ya nchi yetu ambayo ni lango kuu la soko la nchi jirani.

Kampuni hiyo imejipanga kuleta teknolojia ya kisasa inayozingatia hifadhi ya mazingira ("Green Steel"), huku ikishirikiana na wadau wa ndani kukuza ujuzi wa kiufundi kwa wafanyakazi wa Kitanzania.

Ikiwa mradi huu utatimia, utakuwa ni mapinduzi makubwa yatakayopunguza uagizaji wa chuma kutoka nje na kuifanya Tanzania kuwa muuzaji mkuu wa bidhaa hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Maendeleo haya mkoani Mtwara yatachochea ukuaji wa miundombinu na usafirishaji, huku yakitekeleza kwa vitendo azma ya Rais Samia ya kuhakikisha rasilimali za taifa zinamnufaisha mwananchi wa kawaida kupitia mnyororo wa thamani.

Kikao hiki cha Ikulu kimeacha ujumbe mzito kwa ulimwengu wa biashara kuwa Tanzania si tu iko wazi kwa uwekezaji, bali imejipanga kushirikiana na wababe wa teknolojia duniani kuandika historia mpya ya viwanda.

Chapisha Maoni

0 Maoni