Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir bin Ally, ameitaka serikali, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kujenga umoja wa kitaifa, kustahimiliana na kuchukuliana ili kudumisha taifa moja lililo tulivu na imara.
Akizungumza Machi 21, 2026, katika Baraza la Eid el-Fitr kitaifa lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mufti Zubeir amesema Tanzania inaendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kuenzi amani na mshikamano miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali.
Amesisitiza kuwa uhusiano mzuri uliopo kati ya Waislamu na Wakristo ni jambo la kujivunia na limekuwa chachu ya maendeleo ya nchi.
Katika mawaidha yake, Mufti amewataka Waislamu na Watanzania kutunza amani ya nchi, akibainisha kuwa mafundisho ya Kurani yanawaagiza waumini kuitunza nchi yao.
Aliongeza kuwa Muislamu asiyetunza nchi hafuati maelekezo ya Mungu, hivyo amehimiza jamii kuendelea kuishi katika tabia njema ambayo ndiyo mhimili wa mafanikio.
Alitoa mwito kwa wananchi kutokubali kuhadaiwa na maadui wa nje wanaotumia mbinu kuharibu maadili ya Watanzania na kuwahadaa wafanye uovu, akisisitiza kuwa ni lazima kuendelea kuyaishi mema yote yaliyojifunzwa ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Mufti Zubeir pia ametoa angalizo kali kuhusu maendeleo ya sayansi na teknolojia, hususani matumizi ya akili bandia (AI). Amesisitiza umuhimu wa kuitumia teknolojia hiyo kwa uangalifu na uwajibikaji ili kuepuka madhara yanayoweza kuathiri maadili, mshikamano na usalama wa jamii.
Aidha, amekemea vikali mmonyoko wa adabu na nidhamu katika mijadala ya kijamii na kidini, akionya kuwa tabia ya watu wasio na utaalamu kusema maneno ya hovyo dhidi ya viongozi na mamlaka ni njia ya upotofu inayopaswa kuachwa mara moja.
Vilevile, Sheikh Mkuu amekemea matumizi mabaya ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambayo yamegeuka kuwa majukwaa ya kutukana na kukashifu bila hofu ya Mungu.
Amewataka viongozi wa dini kuacha malumbano na mizozo baina yao, na badala yake waelekeze nguvu katika kujenga taifa moja na kuangalia mustakabali wa nchi.
Kauli hizi zinaungwa mkono na Katibu wa Baraza la Maulamaa, Shehe Hassan Chizenga, aliyekumbusha kuwa Watanzania wakidumu katika tabia njema ni baraka kwa taifa na ni njia ya kupendwa na Mwenyezi Mungu.

0 Maoni