Takribani mikoa sita nchini inayopata mvua mara mbili kwa mwaka, ikiwamo Dar es Salaam, inatarajiwa kupokea mvua za wastani hadi juu ya wastani wakati wa msimu wa Masika unaotarajiwa kuanza mwezi Machi, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Januari 5, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a, amesema mvua za Masika zinazojumuisha miezi ya Machi, Aprili na Mei zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi Machi na kuendelea hadi Mei au Juni, 2026 katika baadhi ya maeneo.
Dk. Chang’a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi, hali ambayo inahitaji wananchi na mamlaka husika kuchukua tahadhari mapema ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Kwa mujibu wa wataalamu wa hali ya hewa, ongezeko la mvua linaweza kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu, pamoja na kuongezeka kwa magonjwa yatokanayo na maji kama vile kipindupindu na homa ya matumbo, hasa katika maeneo ya mabondeni na yale yenye mifumo duni ya maji taka.
Mikoa inayotarajiwa kupata mvua hizo ni pamoja na Kagera na Geita, pamoja na maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini ikiwemo mikoa ya Tanga na Morogoro.
Vilevile, Mkoa wa Pwani unatarajiwa kupata mvua za aina hiyo pamoja na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba, ambako wakazi wanashauriwa kuwa waangalifu dhidi ya athari za mvua hizo, ikiwemo mafuriko na kukatika kwa huduma muhimu.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa zitakazokuwa zikitolewa mara kwa mara ili kupata tahadhari za mapema na kuchukua hatua stahiki wakati wa msimu wa mvua.

0 Maoni