Watanzania
wakiadhimisha miaka 64 ya uhuru wa Tanzania Bara wametakiwa kuendelea kuienzi
amani, utulivu na mshikamano vilivyo nguzo kuu za maendeleo, huku wakikataa
kabisa vitendo vya udini na ukabila ambavyo vinaweza kuingiza nchi katika
machafuko.
Huku kukumbushwa
kwa umuhimu wa amani kunakuja wakati baadhi ya watu wanahimiza uharibifu na
vurugu nchini, huku wao wakifurahia maisha ya utulivu katika nchi za nje.
Mwenyekiti wa
Baraza la Ushauri wa Wazee Mkoa wa Pwani, John Kirumbi, amesema nchi yetu
inaongozwa kwa amani na utulivu na mshikamano, akisisitiza: “Tusiruhusu amani
na utulivu vilivyopo kutoweka kwani kuvirudisha gharama yake ni kubwa,
tusikubali kuyumbishwa tuwe na mshikamano.” Kirumbi alihimiza kutoa elimu kwa
vijana ili waweze kuyaenzi mambo haya muhimu kwa mustakabali wa nchi.
Akizungumza kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amewataka wananchi
kuendelea kuilinda amani ya nchi kwa kufuata sheria na kanuni za nchi. “Pia
tulinde utulivu na kutokubali kuvunja utulivu uliopo, tushikamane kwa nguvu
zote kuiletea nchi yetu maendeleo,” alisema Morcase.
Katibu wa Siasa,
Uenezi na Mafunzo CCM Mkoa wa Pwani, Dk David Mramba, aliungana na wito huo
akisema amani ni tunu ya taifa na msingi wa maendeleo. “Watanzania tuendelee
kulinda amani yetu na tusikubali mtu kuivuruga kwani hiyo ni tunu ya taifa letu
na tudumishe utulivu uliopo ili tuweze kusonga mbele kwenye shughuli zetu za
kila siku,” alisisitiza Dk. Mramba.
Aidha, wachambuzi
wa masuala ya jamii wamekumbusha maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, akionya kuwa taifa lisilo na amani huishia katika vurugu.
Wamesema Watanzania hawapaswi kuendekeza udini na ukabila kama vigezo vya
kuwahukumu watu au kupata viongozi, kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha amani na
kujifananisha na mataifa yaliyoingia katika migogoro mikubwa.
Ujumbe wa msingi
unabaki kuwa: Amani na utulivu ni jukumu la kila Mtanzania, na gharama ya
kuvunja utulivu huo ni kubwa mno kwa Taifa.

0 Maoni