Tanzania
imeendelea kung’ara kimataifa baada ya kushinda tuzo ya dunia katika sekta ya
utalii kwa mwaka wa pili mfululizo, ikitambuliwa kama nchi bora zaidi duniani
kwa utalii wa safari. Ushindi huo wa kihistoria unatajwa kuwa ni matunda ya
uongozi bora na juhudi za Serikali katika kuhifadhi na kukuza sekta ya utalii.
Katibu Mkuu Wizara
ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, alieleza hayo hivi karibuni jijini
Dar es Salaam walipopokelewa baada ya kurejea na tuzo tano kutoka
Bahrain-Manama, nchi ya kisiwa iliyopo kati ya Saudi Arabia na Qatar, ambapo
tuzo hizo zilitangazwa.
Mafanikio Yafungua
Milango ya Uenyeji
Dkt. Abbas alisema
kufuatia Tanzania kushinda tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo, mwaka ujao wa
2026, Tanzania imepewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa tuzo hizo za dunia. Tuzo hizo
mwaka jana zilifanyika Ureno na mwaka huu Bahrain.
"Hivyo
mwakani, dunia, mashirika makubwa duniani na wadau wakubwa wa utalii na kampuni
zote kubwa watazifuata tuzo hizo Tanzania," alisema Dkt. Abbas. Aliongeza
kuwa muda wa tuzo hizo utatangazwa hapo baadaye.
Awali, Dkt. Abbas
alisisitiza kuwa tuzo hii ni kubwa katika sekta ya utalii duniani, na
kutambulika kwa Tanzania ni jambo kubwa sana. Aliishukuru Serikali chini ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na marais wengine wote waliopita, kwa kuwekeza nguvu
katika uhifadhi na sekta ya utalii.
Serengeti Yashinda
Hifadhi Bora Duniani
Mkurugenzi Mkuu wa
Bodi ya Utalii Nchini (TTB), Ephraim Mafuru, alishukuru wadau wa sekta ya
utalii kwa michango yao katika kuhakikisha Tanzania inashinda tuzo hiyo.
Alisisitiza kuwa ushindi huo unathibitisha kuwa dunia imetambua ubora wa
vivutio vya utalii vya Tanzania.
Mafuru alipongeza
hususani Hifadhi ya Serengeti ambayo ilishinda tuzo ya Hifadhi Bora Duniani.
Alisema Tanzania ina mafanikio makubwa katika uhifadhi, kwa sababu sio tu nchi
yenye vivutio vya wanyamapori bali maeneo mengi ya kipekee, ikiwemo mapori ya
akiba na misitu.
Aliongeza kuwa
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii, ikiwa ni
pamoja na ujenzi wa barabara katika maeneo ya hifadhi.
Wito wa Amani na
Utulivu
Mafanikio haya
yanatumika kama mfano wa jinsi matunda ya uongozi bora, utulivu, na amani
yanavyoweza kukuza Taifa kiuchumi. Watanzania wanahimizwa kuendelea kuwa
wapole, kujenga Taifa, na kuacha tabia ya kujutia kwa kufuata uchochezi, kwani
maendeleo haya yanahitaji utulivu wa kudumu.

0 Maoni