Wananchi wa Kitongoji ya Ormekeke Kijiji cha
Nasipaoriong tarafa ya Ngorongoro wameanza kunufaika na mradi wa maji baada ya
Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuchimba kisima chenye uwezo
wa kuzalisha lita 13,00 kwa saa na kujenga tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji
lita 135,000 kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo.
Akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa
mradi huo Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Abdul-Razaq Badru ameeleza kuwa
kukamilika kwa mradi huo kümeleta manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo ya
Ormekeke, Nasipaoriong na Olduvai yaliyopo hifadhi ya Ngorongoro ambao kipindi
cha kiangazi walilazimika kuhamishia mifugo maeneo ya mengine kufuata maji.
“Mradi huu tuliuanza kwa kuwashirikisha
wananchi ikiwa ni utekelezaji wa kuboresha mahusiano ya NCAA na jamii kwa
kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ambalo moja wapo ni maji,
umeshakamilisha na kitongoji cha Ormekeke wameanza kutumia maji, rai yangu kwa
wananchi ni kulinda na kusimamia miundombinu ya mradi huu kupitia kamati za
maji na mazingira ambazo wameshaziunda” alisema Kamishna Badru.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ormekeke Bw. Oreteti Olenjorio ameeleza kuwa eneo la
kitongoji hicho ni kame na halina chanzo chochote cha maji hivyo uamuzi wa
Serikali kupitia mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kuchimba maji ni msaada
mkubwa kwa matumizi ya wananchi na mifugo na kuahidi kulinda miundombinu ya
mradi huo kupitia jumuiya za maji na kuzingatia sheria za hifadhi.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi
Godlove Sengele pamoja na mradi huo kunufaisha wananchi na mifugo yao pia
utahudumia Makumbusho ya Olduvai, Leakey Camp, Mtui Camp, Nyumba za Maaskari
pamoja na jamii ambayo imejengewa vituo vinne vya kuchotea maji na vituo vitatu
vya kunyweshea mifugo.




0 Maoni