Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Boniface Simbachawene,
ametoa wito mzito kwa wananchi, hasa kundi la vijana, kudumisha amani na
kuepuka kabisa kushiriki katika mipango ya maandamano, akisema nchi bado
inakabiliwa na athari kubwa za vurugu za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Waziri Simbachawene alitoa kauli hiyo Novemba 28, 2025, wakati wa hafla
ya burudani ya amani iliyofanyika katika Soko la Nyama Choma la Kumbilamoto,
Vingunguti, Dar es Salaam.
Akikumbusha matukio ya mwaka 2025, Mhe. Simbachawene alibainisha kuwa
vurugu zilizofuata uchaguzi huo zilisababisha hasara isiyopimika, ikiwemo vifo,
uharibifu mkubwa wa mali za umma na watu binafsi, pamoja na kusimama kwa
shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali.
Tahadhari Desemba 9
Waziri alionya kwamba Serikali inazo taarifa za mipango ya vurugu
inayotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2025. Alisisitiza msimamo wa Serikali kwamba
haitaruhusu vurugu zozote kutokea, na akawaomba wananchi kutotumika na kuchochewa
kurudia makosa yaliyopita.
“Ni lazima vijana wetu wafahamu gharama kubwa ya uharibifu. Kuchoma vituo
vya mabasi ya mwendokasi—mradi uliojengwa kwa ajili ya wananchi wasio na
uwezo—ni kujijengea deni,” alisema Simbachawene. Alifafanua kuwa miradi hiyo
inagharamiwa na kodi na mikopo ambayo vizazi vijavyo vitapaswa kuilipa.
Umuhimu wa Kujifunza kwa Majirani
Akisisitiza thamani ya utulivu, Waziri alisema Tanzania inaonekana
kuonewa wivu kutokana na amani na mafanikio yake. Aliwataka wananchi kujifunza
kutoka kwa nchi jirani zinazokumbwa na migogoro ya muda mrefu.
Alitoa mfano wa wakimbizi wa Burundi waliodumu nchini kwa karibu miaka
40, ambao Serikali sasa inashauriana na UNHCR (Shirika la kuhudumia wakimbizi
duniani) namna ya kuwashawishi warudi kwao.

0 Maoni