Mtaalamu wa masuala ya jamii, Dkt. Francis Daudi, ametoa
onyo kali kuhusu athari mbaya za vurugu zinazojitokeza wakati wa chaguzi,
akisisitiza kwamba "vurugu zinazojitokeza katika chaguzi nyingi duniani
huwa hazileti suluhisho la kudumu, bali husababisha athari zinazodumu kwa muda
mrefu."
Dkt. Francis ambaye ni mwanahistoria alifafanua kuwa ghasia
wakati wa uchaguzi huathiri moja kwa moja shughuli za kiuchumi za taifa.
Alieleza, "vurugu wakati wa uchaguzi huwazuia wananchi kushiriki
kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali, hali inayosababisha kudorora kwa
uchumi kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi taifa kwa ujumla."
Mbali na kudorora kwa uchumi, Dkt. Francis alieleza kuwa
athari za vurugu hizo ni pamoja na upotevu wa maisha (vifo), hasa kwa wale
ambao ni nguzo na tegemeo katika familia na jamii. Alisisitiza kuwa hali hiyo
hupelekea familia zilizoachwa kuingia katika umasikini, utegemezi, na kupoteza
nguvu kazi – mambo ambayo huacha makovu ya kijamii yanayodumu.
Maoni ya Dkt. Francis yamewafanya wananchi wengi kutumia
majukwaa ya mitandaoni kuunga mkono wito wa amani na utulivu. Baadhi ya maoni
yaliyoonekana kuunga mkono ujumbe huo ni pamoja na:
@mussa.lameck_ alisisitiza umuhimu wa kushughulikia mizizi
ya matatizo kabla hayajageuka kuwa vurugu, akisema, "Haitakiwi watu
kuachwa na vitu moyoni hadi vitoke kwa kufanya vitendo vya kihalifu, tuilinde
Amani yetu kwa kuzingatia mahitaji na sauti za wananchi maskini kwa
wakati."
@cdekibua alipongeza vijana kwa kuepuka kuchochewa,
akisema, "Amani imeshinda... Vijana wa Tanzania tumethibitisha kuwa nguvu
yetu kubwa si vurugu, bali busara, umoja na upendo kwa taifa letu."
Alihitimisha kauli yake hiyo na hashtag ya NCHIKWANZA.
@bulugumagege alitoa wito wa kitaifa akisema, "Ni
Kweli Kama Taifa Tuendelee Kuwa Wamoja Na Kuitunza Amani Yetu Ili Tuweze
Kusonga Mbele Kams Taifa."
Ujumbe huu unaotokana na majadiliano yaliyotokea katika
Jukwaa la Wachambuzi unaongeza uzito katika mijadala inayoendelea nchini kuhusu
jinsi ya kudumisha utulivu wa kisiasa na kuimarisha ushirikishwaji ili kuepuka
athari za ghasia katika mzunguko wa uchaguzi.

0 Maoni