Vijana
wanahimizwa kutambua na kufuatilia kwa karibu mipango ya serikali, hasa hatua
za kuboresha vituo vya maendeleo ya vijana. Kwa kutumia vituo hivi, vijana
wanaweza kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira na kuanzisha
miradi yao wenyewe, na hivyo kutengeneza fursa za ajira kwao na kwa wengine.
Wito
huo umetolewa wakati Serikali ya Tanzania imeainisha dhamira yake thabiti ya
kuviboresha na kuvitumia kikamilifu vituo vya maendeleo ya vijana nchini ili
viwe silaha muhimu ya kuwawezesha vijana kiuchumi, kijamii, na kielimu.
Desemba
15, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana,
Mhe. Joel Nanauka, akitembelea na kukagua utendaji kazi katika Kituo cha Vijana
cha Sasanda kilichopo mkoani Songwe alibainisha kuwa kuna jumla ya Vituo vitatu
vikuu vya Vijana nchini, vya Sasanda (Songwe), Ilonga (Morogoro), na Marangu
(Kilimanjaro).
"Kituo
hiki cha Sasanda kilitoa mafunzo kwa vijana tangu mwaka 1979 na mara ya mwisho
kufanya hivyo ilikuwa mwaka 2008. Kwa muda mrefu kimekuwa hakifanyi kazi. Ndiyo
maana tumejipanga kuviboresha vituo hivi na kuhakikisha vinawasaidia vijana
katika maeneo haya," alisema Mhe. Nanauka.
Alisisitiza
viongozi wa mikoa ambako vituo hivi vipo kuviweka katika kipaumbele, akieleza
kuwa ni maeneo yenye mazingira bora na fursa sahihi kwa vijana.
Waziri
alikumbusha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, imetoa kipaumbele kikubwa kwa masuala ya Maendeleo ya Vijana,
kiasi cha kuamua kuunda Wizara maalumu inayoshughulika na mambo yao. Hatua hii
inaonyesha uwekezaji mkubwa wa Serikali katika mustakabali wa vijana.
Kwa
upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana, Dkt.
Kedmon Mapana, aliwakumbusha Watendaji wa Serikali kuendana na falsafa za
Wizara, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kasi, kutembelea maeneo
wanayopatikana vijana, na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kufanikisha
miradi ya vijana.

0 Maoni