Katika hali inayoshiria kukomaa kwa fikra za kimaendeleo
miongoni mwa vijana, mbunifu Thomas Ryoba amezindua huduma ya vituo vya kukodi
kuchaji simu iitwayo “Smart Chaja,” mfumo unaomwezesha mteja kukodi power bank
kupitia programu tumizi ya simu pindi anapopata dharura.
Ryoba amesisitiza kuwa huduma hiyo itapatikana katika
maeneo rasmi kama ofisi, hospitali, na kumbi za starehe, huku akiwahimiza
vijana wenzake kuchangamkia fursa za ubunifu ili kujipatia kipato na kufikia
ndoto zao.
Hata hivyo, wadau wa maendeleo wamebainisha kuwa ubunifu
kama huu wa Ryoba unahitaji mazingira tulivu na salama ili uweze kustawi na
kuvutia wateja.
Maoni ya wananchi mtandaoni yamepongeza hatua hiyo kama
"akili kubwa," yakisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia teknolojia
kujenga uchumi badala ya kuitumia kama chombo cha kuvuruga utulivu. Amani
imetajwa kuwa nguzo muhimu inayowezesha sekta binafsi na wabunifu wadogo kukua
na kuchangia katika malengo ya serikali ya kukuza viwanda na ajira.
Wananchi wamehimizwa kulinda amani ili kutoa nafasi kwa
wabunifu hawa kufanya kazi bila hofu ya uharibifu wa mali kama ilivyowahi
kutokea mnamo Oktoba 29, ambapo baadhi ya makampuni yalichomwa moto wakati wa
vurugu.
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi
kuwa hali ya usalama ni shwari, jambo linalotoa fursa kwa biashara na ubunifu
mpya kama wa "Smart Chaja" kuendelea msimu huu wa sikukuu.

0 Maoni