Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kali na la wazi kwa wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu na uharibifu kwa kisingizio cha ‘maandamano ya amani yasiyo na kikomo’ kuanzia tarehe 9 Desemba 2025. Kwa mujibu wa Jeshi hilo, uhamasishaji huu unalenga kuvuruga amani na maisha ya wananchi.
DCP David Misime,
Msemaji wa Jeshi la Polisi, amethibitisha kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama
vinafuatilia kwa karibu mipango hii hatarishi. Jeshi linaendelea kutekeleza
majukumu yake ya msingi ya kulinda maisha na mali, huku likiimarisha hali ya
amani, utulivu na usalama nchini.
Taarifa ya Jeshi
la Polisi inaonyesha kuwa uhamasishaji unaoendelea katika makundi sogozi
unalenga kufanya vitendo vitakavyosimamisha nchi na kuingiza taifa katika
machafuko:
Wahamasishaji
wanawataka washiriki kuharibu na kuchoma moto minara yote ya mawasiliano ili
nchi nzima ikose mawasiliano. Pia, wanapanga kufunga Bandari ya Dar es Salaam
kwa kuzuia barabara zote za kuingia na kutoka bandarini, hivyo kuzuia shughuli
za kiuchumi.
Mipango inahusisha
pia kufunga mipaka yote ya nchi ili kuzuia mtu yeyote asitoke au asiingie
nchini. Jambo linalotia hofu zaidi ni kwamba wahamasishaji wanahamasishana siku
hiyo waende hospitalini kuzuia huduma kwa wagonjwa zisitolewe, kwa lengo la
kulifanya Taifa lisimame kabisa.
Kwa upande wa
usalama wa raia, uhamasishaji unawataka vijana wakapore mali za watu kwa
kisingizio kuwa wana njaa. Pia, kuna matamko kwamba watakwenda kuwafuata
watumishi wa Serikali popote walipo ili kuwadhuru. Wakati wa uhamasishaji huo,
viongozi wa maandamano hayo wanaelekeza kwamba ambaye hajui kutumia silaha na
hajapitia mafunzo siku hiyo asishike silaha, awaachie waliopata mafunzo ya
matumizi ya silaha.
Katika kukabiliana
na miito hiyo ya uharibifu, Jeshi la Polisi linawapongeza na kuunga mkono
wananchi na vijana wanaopenda amani ambao tayari wameahidi kulinda amani katika
maeneo yao.
Amani siyo maneno
ni kazi. Vijana, kama walinzi wa Taifa, wanahimizwa kukataa kuwa vibaraka wa
kisiasa. Katika matamko yanayopinga vurugu, wengine wameapa na kutamka kuwa
watakaokwenda kuandamana wasifike kwenye mitaa yao kwani watawashughulikia
ipasavyo. Wengine wanasema hawatakubali tena kupata hasara waliyoipata Oktoba
29 na siku zilizofuata, hivyo watahakikisha kuanzia Desemba Tisa wanalinda
maisha, familia, na mali zao.
DCP Misime
amewahakikishia wananchi wote wapenda amani kuwa Jeshi la Polisi na vyombo
vingine vya ulinzi na usalama vipo tayari kulinda maslahi ya Taifa. Wale wote
wanaohamasisha vurugu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wananchi
wamekumbushwa kuwa mwezi huu wa Desemba ni kipindi cha maandalizi ya sherehe za
mwisho na mwanzo wa mwaka. Jeshi linawahimiza wananchi kuendelea na maandalizi
mazuri yanayozingatia usalama wa maisha na mali zao, na wanahimizwa kuzingatia
sheria za usalama barabarani.
Amani na Utulivu
wa Tanzania utaendelea kuimarishwa, na hakuna mwananchi atakayeruhusiwa
kusumbuliwa katika shughuli zake za kila siku.

0 Maoni