Tanzania imejikuta
katikati ya vuta-nikuvute ya kidiplomasia kufuatia matamko na hatua za baadhi
ya nchi washirika wa maendeleo baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025. Huku
Serikali ikisisitiza umuhimu wa Tume ya Uchunguzi kutoa majibu sahihi, hatua ya
baadhi ya mataifa kutishia au kukata misaada inazua mjadala mzito kuhusu uhuru
wa nchi kujitathmini na tabia ya mataifa rafiki kutaka kuingilia masuala ya
ndani.
Mchambuzi
mashuhuri wa siasa na jamii, Maggid Mjengwa, anatoa nuru mpya juu ya hatua za
Sweden, akibainisha kuwa uamuzi wa kukata misaada kwa Tanzania na nchi nyingine
tano (ikiwemo Msumbiji na Zimbabwe) haukutokana na matukio ya hivi karibuni,
bali ni suala la kiitikadi na maslahi ya kitaifa ya Sweden.
"Ilitarajiwa,
na... haitokani na matukio ya hivi karibuni nchini Tanzania," anasema
Mjengwa. "Sababu ya msingi ya kuifutia misaada Tanzania ni Sera za
Kijamaa... Tatizo ni Ujamaa wa Tanzania."
Mjengwa anasema
wazi kwamba Serikali ya sasa ya Sweden, yenye mrengo wa Kihafidhina, inachukia
Sera za Kijamaa za Tanzania zilizowekwa tangu 1962. Kinachoshangaza zaidi,
fedha hizo sasa zimeelekezwa Ukraine, ikithibitisha kwamba misaada inafuata
vipaumbele vya usalama na maslahi ya taifa la mtoaji (Sweden), na siyo umaskini
wa mpokeaji.
Hatua hii ya
Sweden na matamko ya baadhi ya nchi za Magharibi kuhusu matukio ya ndani ya
Tanzania, yanaibua swali la msingi: Je, misaada ya maendeleo ni kweli kusaidia
umaskini, au ni njia ya kuingiza ajenda za kisiasa?
Inaonekana kuna
tabia inayoendelea ya mataifa rafiki kutaka kuweka viwango vya maadili vya juu
zaidi kwa nchi zinazoendelea kuliko vile wanavyojiwekea wao wenyewe. Matamko
yanayotolewa baada ya matukio kama yale ya Oktoba 29 yanaonekana kuwa na lengo
la kuishinikiza Serikali kufanya maamuzi yanayokidhi matakwa ya kigeni, badala
ya kuheshimu mchakato wa uchunguzi wa kitaifa.
Kwa upande
mwingine, Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa inatambua mchango wa washirika
wa kimataifa katika demokrasia, lakini imewataka wadau wote kusubiri matokeo
rasmi ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa kwa kuwa Tanzania ni nchi ina haki kamili
ya kutumia mifumo yake ya kisheria na kitaasisi kujichunguza yenyewe kabla ya
kupokea hukumu za nje. Pia mahusiano ya kimataifa yanapaswa kuendelezwa katika
msingi wa heshima ya usawa, na si uhusiano wa mtoaji na mpokeaji wa amri.
Kama Mjengwa
anavyokumbusha, Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitupitisha
kwenye njia ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo ilitupa uwezo wa kujihami
kiitikadi. Hotuba ya Rais, wakati akifungua Bunge, zimethibitisha hali hii ya
majaribu kwa kutoa wito kwa Watanzania kujifunga vibwebwe.
Wito wa kiongozi
wa nchi wa kusisitiza kuwa matajiri wanakata misaada unaakisi maono ya zamani
ya Nyerere. Ujumbe wake ni wazi: Taifa linapaswa kuzunguka bendera ya Taifa na
kulinda umoja wake dhidi ya mbegu za utengano, kwani hakuna nchi nyingine ya
kukimbilia.
Ni wakati sasa,
kama Mjengwa anavyohimiza, kwa Watanzania kufanya Tafakuri Jadidi juu ya
mwelekeo wa Taifa letu. Uhuru wa kutoa maamuzi bila kushinikizwa na misaada
ndiyo kiini cha uhai na utambulisho wetu kama Taifa huru.

0 Maoni