TBN yatoa wito wa Amani, Tanzania ikiadhimisha Miaka 64 ya Uhuru

 

Tanzania Bloggers Network (TBN) imetoa salamu maalumu kwa Watanzania katika kuadhimisha miaka 64 ya Uhuru leo, Desemba 9, ambapo imesisitiza umuhimu wa kutafakari safari ya maendeleo ya Taifa na nafasi ya kila Mtanzania katika kuendelea kulijenga.

Akitoa salamu hizo, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, amesema kuwa siku ya Uhuru si tukio la mapumziko pekee, bali ni siku ya kukumbuka misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa katika kutafuta, kudumisha na kulinda Uhuru wa Tanzania.

Msimbe aliwakumbusha Watanzania kauli ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusisitiza kuwa Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea.

“Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama tunategemea wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi,” alimnukuu Mwalimu Nyerere.

Amani na Utulivu: Nguzo za Maendeleo

TBN imeeleza kuwa mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika miaka 64 ya Uhuru yametokana na misingi ya amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Msimbe alisema kuwa bila misingi hiyo, jitihada za Taifa katika kushughulikia changamoto za ujinga, umaskini na maradhi haziwezi kufanikiwa.

Akinukuu maneno ya Rais mstaafu Benjamin William Mkapa, Msimbe alisema:

“Amani si kitu cha asili, tunahitaji kuilinda na kuitunza kila siku. Bila amani, hakuna maendeleo ya kweli.”

TBN imeonya kuwa vurugu na uchochezi vyaweza kudhoofisha jitihada za kizazi kilichopita na kizazi cha sasa katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Kila Kizazi na Zama Zake

Katika salamu hizo, TBN pia iligusia umuhimu wa kuheshimu zama tofauti za uongozi, ikinukuu kauli maarufu ya Rais Mstaafu Hayati Ali Hassan Mwinyi:

“Kila utawala na zama zake. Kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa Taifa hili.”

Mwenyekiti huyo alisema kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchi inaendelea kusimamia dira ya 4R  Reconciliation, Resilience, Reforms, and Rebuilding  ambayo inalenga kuimarisha maridhiano, mageuzi na ustawi wa Taifa.

Wito kwa Watanzania

TBN imewataka Watanzania kutumia uhuru wa kujieleza kwa kujenga, si kubomoa, kwa kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, kudumisha amani na kuepuka kutumika kama chombo cha kuchochea migawanyiko.

“Watanzania, tunayo nafasi ya kuzungumza, tuzungumze. Tusiitumie nafasi hiyo kubomoa Taifa bali kulijenga,” alisema Msimbe.

TBN imemalizia kwa kuwatakia Watanzania wote maadhimisho mema ya miaka 64 ya Uhuru, ikimalizia na kauli mbiu:

Tanzania Kwanza, Kazi na Utu Tusonge Mbele

Chapisha Maoni

0 Maoni