Licha ya kuwepo
kwa kampeni za uchochezi na miito ya kutatiza amani inayosambazwa, hasa kwenye
mitandao ya kijamii, jamii ya kimataifa imedhihirisha imani yake thabiti kwa
Tanzania, ikisisitiza kuwa nchi inaendelea kuwa mahali salama na pa kuaminika
kwa mikutano mikubwa na uwekezaji.
Ushahidi wa hivi
karibuni ni kuchaguliwa kwa Arusha kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Umoja wa Mabunge
Duniani (IPU), tukio la kihistoria linalotarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe zaidi
ya 1500.
Mwaliko huu maalum
unamfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo muhimu unaokusanya Maspika,
Wabunge, na viongozi mbalimbali kutoka nchi wanachama wa IPU.
Mwaliko wa IPU
Uthibitisho wa Amani
Uteuzi wa Tanzania
kuwa mwenyeji wa mkutano huu unasisitiza uhusiano mzuri wa kimataifa
unaoendelezwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaochangia kufungua fursa
nyingi za kiuchumi na uwekezaji.
Akipokea Ujumbe wa
IPU ulioongozwa na Balozi Ande Filip, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA. Amos
Gabriel Makalla, alisisitiza umuhimu wa tukio hili kwa Taifa. "Tanzania ni
Mwenyeji na sababu kubwa ni ushiriki na historia yake katika IPU na kikubwa
zaidi ni namna wao wanavyoiona Tanzania," alisema Mhe. Makalla.
Mhe. Makalla
alibainisha kwamba mkutano huu unakuja wakati mzuri katika kudhihirisha amani,
usalama na utulivu uliopo nchini na kuaminika kwa Tanzania Kimataifa. Hii
inathibitisha kuwa, tofauti na propaganda za uchochezi, dunia bado inaiona
Tanzania kama nchi yenye utulivu.
Fursa Kubwa za Kiuchumi na Utalii
Balozi Ande Filip,
kwa niaba ya ujumbe wa IPU, alieleza kuwa mkutano huo utafanyika kwa siku sita
Jijini Arusha, na washiriki wake watakuwa na zaidi ya siku sita Mkoani Arusha
ili kutembelea maeneo ya kihistoria na vivutio vya utalii.
Mhe. Makalla
aliwataka wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kujiandaa kutumia fursa
kubwa za kiuchumi zitakazoletwa na ujio wa wageni hawa. Ujumbe wa wajumbe zaidi
ya 1500 una maana ya kuongezeka kwa mahitaji ya huduma, ikiwemo malazi,
usafiri, na manunuzi. Hii inatafsiriwa kuwa faida ya moja kwa moja kwa
wafanyabiashara wadogo na sekta ya utalii, ikionyesha faida halisi za utulivu
wa ndani.
Watanzania
wamehimizwa kudumisha amani na umoja wao, kwani utulivu wa ndani ndio ufunguo
wa kuendelea kuleta maendeleo na kuvutia fursa zaidi za kiuchumi na kuaminika
kimataifa.

0 Maoni