Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) Bw. Abdul-Razaq Badru amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kufanya kazi
kwa bidii, weledi, uamunifu, ubunifu na ushirikiano katika ulinzi wa
rasilimaliza za Wanyamapori na misitu ili kuenzi uhuru wa Tanzania Bara kwa
vitendo.
Katika salamu zake za kuadhimisha miaka 64 ya Uhuru
wa Tanzania Bara kamishna Badru amesema hifadhi ya Ngorongoro imedhamiria
kuendelea kuwa eneo muhimu la uhifadhi na utalii duniani na kusisitiza kila
mtumishi kutimiza majukumu yake kwa malengo ya kimkakati na kutekeleza dira ya
nchi ya 2050.
“Dhamira yetu kwa Ngorongoro ni kuendelea kuifanya
kuwa Premium Safari Destination hivyo hatutomwacha mtu nyuma wala kukata tamaa
katika kutimiza malengo hayo na tutahakikisha tunalinda rasilimali za
Wanyamapori, misitu na malikale zilizopo Ngorongoro kwa wivu mkubwa kama ambayo
mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere alituachia,”alisema Kamishna
Badru.
Ameeleza kuwa katika maadhimisho haya ya miaka 64 ya
uhuru wa Tanzania bara njia pekee ya Ngorongoro kuyaenzi ni kuongeza ufanisi katika
nyanja zote za uhifadhi,utalii na kudumisha mahusiano thabiti kwa maendeleo ya
jamii.
Katika kuadhimisha siku ya uhuru wa Tanzania Bara
Maafisa na askari wa Jeshi wa Uhifadhi Ngorongoro wametumia siku hiyo kufanya
usafi katika maeneo mbalimbali yaliyopo eneo la hifadhi ya Ngorongoro ili
kuendelea kuweka mandhari ya kuvutia kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.
Tanzania bara inaadhimisha miaka 64 ya uhuru
uliopatikana tarehe 09 Desemba mwaka 1961 chini ya uongozi thabiti wa baba wa Taifa hayati Julius
Kambarage Nyerere.

0 Maoni