Rais Samia atoa msamaha kwa wafungwa, aachia huru 22

 

Katika kusherehekea miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania Bara hii leo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza msamaha kwa wafungwa 1,036 baadhi akiwapunguzia adhabu na wengine kuwaachia huru.

Kati ya wafungwa hao waliopata msamaha huo wa Rais, 22 wameachiwa huru, huku 1,014 wakipunguziwa adhabu zao na watakabaki gerezani kutumikia sehemu ya vifungo vilivyobaki.

Msamaha huo wa Rais kwa wafungwa, hutolewa Desemba 9, kila mwaka. Mkuu wa nchi chini ya ibara ya 45(1)(a)-(d) ya Katiba ya Tanzania, amepewa mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa.

Taarifa ya msamaha huo, imetolewa leo Desemba 9, 2025 na Wizara ya Mambo ya Ndani na kutiwa saini na Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene.

Katika taarifa hiyo, Simbachawene amesema ni matarajio ya Serikali kuwa wafungwa walioachiwa huru watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee gerezani.

Idadi ya wafungwa walioachiwa huru leo Desemba 9, 2025 inafanana na ile ya waliochiwa katika msamaha wa Rais wakati wa sherehe za uhuru za mwaka jana.

Chapisha Maoni

0 Maoni