Katika mwendelezo
wa wito wa kudumisha amani na utulivu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,
2025, na wakati kukiwa na wito wa baadhi ya wachochezi mtandaoni kuitisha maandamano mnamo Desemba 9, sauti za
viongozi, wananchi wa kawaida, na Taasisi za kidini zinaendelea kusisitiza kuwa
vijana wanapaswa kukataa kugawanywa na kutumiwa kwa maslahi ya wengine.
Wito huu unakuja
wakati Umoja wa Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) ukitaka Serikali, viongozi
wa dini, vijana na jamii kwa ujumla kuanza safari mpya ya maridhiano baada ya
kadhia ya Oktoba 29 iliyoacha majeraha makubwa.
Sauti ya Mkulima:
Sirio Msimbe,
mkazi wa Tchenzema Mgeta mkoani Morogoro na mkulima, ametoa ushuhuda wake
akielezea jinsi vurugu za Oktoba 29 zilivyogusa moja kwa moja maisha ya
Watanzania maskini.
"Maandamano
ni adui wa taifa na adui wa maisha ya Watanzania maskini," alisema Sirio
Msimbe kwa uchungu. "Vurugu zinasababisha mazao ya wakulima kama mimi,
malimbichi, kukosa soko na kutengeneza hasara kubwa."
Msimbe alieleza
kuwa wakati wa vurugu za Oktoba 29, zaidi ya tani mbili (2) za mazao
yanayoharibika kwa haraka kama brokoli na maharagwe mabichi iliharibika
kutokana na kukosekana kwa usafiri wa kwenda kwenye masoko. Alisisitiza kuwa
wenye vyombo vya usafiri wanaposhindwa kusafirisha bidhaa kwa hofu ya vyombo
vyao kuchomwa, kama ilivyokuwa Oktoba 29, wananchi wanakuwa kama wanakaanga
maisha yao wenyewe.
"Vijana
msikubali kuingia mtaani wala kufanya vurugu. Wengi wetu tunaingia kwa mkumbo
tu kuwezesha maslahi binafsi ya watu," alihimiza Msimbe na kusema kufanya
vurugu ni kuikasirisha dola na pia kuharibu mifumo ya maisha ambayo tayari
inategemeana.
Wito wa JMAT:
Umoja wa
Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) ulitoa tamko rasmi likielezea tukio la
Oktoba 29, ambalo lilisababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali za umma na
binafsi pamoja na taharuki ya kitaifa, kama “jeraha la kitaifa linalohitaji
uponyaji wa pamoja, hekima na majadiliano ya kina.”
Katika mkutano wa
JMAT, Mchungaji Richard Hananja alitoa maneno ya hekima yaliyogusa
wengi:“Changamoto zikitokea, hekima ni kumaliza changamoto bila kuzalisha
changamoto nyingine. Maelewano yanapatikana kwa kiti na meza.”
Kauli hii
inasisitiza ukweli kuwa njia ya mabadiliko ya dunia ya leo si mabavu, si
hasira, si midomo yenye makali—ni mazungumzo, maridhiano, na kusikilizana kwa
uaminifu.
Mchungaji Hananja
aliongeza kuwa safari ya maisha, hususan safari ya mabadiliko, inahitaji jamii
inayowezesha mazungumzo kuanzia ngazi za chini. Alishauri: “Hawa vijana wetu
tukae nao kuanzia chini.”
Kuhusu changamoto
ya ajira inayowakabili vijana wengi, Mchungaji Hananja alikumbusha ukweli wa
msingi: "Elimu ndiyo uwekezaji mkubwa. Elimu ndiyo mbolea ya akili...
Ukiwa na Elimu hushindwi.”

0 Maoni