Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali haitasita
kuchukua hatua dhidi ya jaribio lolote la kuendeleza maandamano au machafuko
nchini, akibainisha kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonesha baadhi ya
waandaaji wa vurugu wamekuwa wakibadili tarehe za mipango yao.
Akizungumza na Wazee wa Jiji Dar es Salaam, Rais Samia
alifichua kuwa mmoja wa wahusika wa mpango huo ameshauri kikundi chake kuepuka
tarehe 9 Desemba na badala yake kuelekeza maandamano yao tarehe 25 Desemba.
“Nataka niwaambie, wakati wowote wakija—tumejipanga,”
alisema Rais Samia.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakituma ujumbe serikalini
wakitoa masharti ya kufanya mazungumzo, lakini akasisitiza kuwa serikali
haitalazimishwa kuchukua maamuzi kinyume na misingi ya uhuru wa taifa.
“Serikali hii haiwezi kuamrishwa. Sisi ni nchi huru,”
aliongeza.
Katika kuelezea presha kutoka kwa baadhi ya makundi, Rais
Samia amesema kumekuwa na shinikizo la “kumuachia mtu fulani” kama sehemu ya
masharti ya maridhiano. Hata hivyo, amesema maridhiano ya kweli hayawezi
kujengwa juu ya mashinikizo kutoka nje bali kupitia utashi wa Watanzania
wenyewe.
Akimnukuu ushindi wa CCM katika uchaguzi uliopita, ambao
aliusema uliifikia asilimia 97, Rais Samia aliwajibu wanaohoji kiwango hicho
akisema:
“Wanaouliza kwa nini asilimia hiyo ni kubwa, hawakuwepo
kwenye uchaguzi. Hawapaswi kutilia shaka maamuzi ya waliojitokeza kupiga kura.”
Ametumia nafasi hiyo kuhimiza umuhimu wa majadiliano na
mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa licha ya majeraha ya kisiasa yaliyowahi
kutokea, Watanzania wenyewe ndiyo wenye uwezo wa kuyaweka sawa kupitia majukwaa
ya mazungumzo, hekima za wazee, na kuwaongoza vijana kutoshirikishwa katika
mipango ya uchochezi.
“Tukae tuzungumze. Wazee wetu na vijana wetu wasitumike.
Tanzania itajengwa na Watanzania,” amehitimisha.

0 Maoni