Viongozi wa dini na watumishi wa
Mungu nchini wamewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, kutumia mitandao ya
kijamii kwa faida chanya, na kupuuza miito yoyote ya kuandamana, hususan ile
inayolenga tarehe 9 Desemba.
Akizungumza hivi karibuni, Askofu wa
Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Sehaba, alisisitiza
umuhimu wa mitandao ya kijamii kama 'baraka' ambayo inaweza kutumika kuhubiri
Injili, kutoa mafundisho, na kuiweka jamii katika maadili.
"MITANDAO ya kijamii ni baraka
na inaweza kutusaidia Kanisa kuhubiri Injili, kutoa mafundisho na kuiweka jamii
katika maadili," alisema Askofu Sehaba.
Hata hivyo, Askofu Sehaba alionya
kuwa mitandao hiyo inaweza kuwa 'janga' kwa jamii endapo itatumika vibaya.
"Nikiwa kiongozi wa dini ningeomba watu wote tunaotumia, tuitumie kuleta
faida chanya kwa Watanzania," alisisitiza.
Kauli yake iliungwa mkono na
Katekista wa Kanisa la Anglikana, Parishi ya Kisaki – Nyalutanga, Wilaya ya
Morogoro, Joshua Msagala, ambaye alitilia mkazo uhusiano kati ya amani na
injili ya wokovu.
"TUNAPOHUBIRI habari ya wokovu
lazima amani iwepo na ndio maana hata ujio wa Yesu Kristo, jambo la kwanza
kulikuwa na amani," alisema Katekista Msagala. "Sisi vijana wanakwaya
tutajitahidi kutunga nyimbo zenye kuhamaisha amani."
Aidha, Mkurugenzi wa Hospitali ya
Berega, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Mchungaji Canon Mgeya, alisisitiza
umuhimu wa kuombea viongozi na kudumisha ulinzi wa amani ya nchi.
"Ni muhimu kwa wananchi kulinda
amani ya nchi yetu na pia kuwaombea viongozi wa serikali akiwemo Rais Samia
Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri Mkuu Dk Mwingulu
Nchemba, mawaziri na viongozi wote wenye mamlaka katika nchi yetu ili kwa
pamoja watuongoze katika haki na kweli," alihitimisha Mchungaji Canon
Mgeya.
Viongozi hao wa dini wametoa wito kwa
umma kupuuza taarifa za uchochezi na miito ya kuandamana iliyosambazwa kupitia
mitandao ya kijamii inayolenga kufanya ghasia, hususan Desemba 9, na badala
yake kuelekeza nguvu katika shughuli za maendeleo na matumizi mazuri ya teknolojia.

0 Maoni