Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kuanza
kwa mchakato mpana wa mapitio ya kanuni, sheria, na ada za leseni zinazosimamia
vyombo vya habari vya mtandaoni. Hatua hiyo ni mwitikio wa moja kwa moja kwa
malalamiko ya muda mrefu ya wadau wa habari nchini ambao wamekuwa wakidai kuwa
mfumo wa sasa unakandamiza ubunifu na unaua ajira kwa vijana.
Akizungumza katika kikao kazi kizito kilichowakutanisha
viongozi wa Serikali , mabloga na waandishi wa habari mtandaoni, Mkurugenzi
Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari, alisema Serikali imekubali "kusikia
kilio" hicho.
Dkt. Bakari alibainisha kuwa kikwazo kikubwa kimekuwa ni
gharama kubwa za leseni na urasimu wa kikanuni ambao umekuwa ukiwafanya
waandishi wengi kushindwa kurasimisha kazi zao. Ili kuhakikisha suluhu ya
kudumu inapatikana, amewaelekeza wadau kupitia TBN na JUMIKITA kuteua wajumbe
wanne watakaoungana na jopo la wataalamu wa TCRA kuandaa mapendekezo ya mabadiliko
ya ada na sheria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe,
aliwasilisha uchambuzi wa kina unaoonyesha jinsi Tanzania ilivyokuwa na
vizingiti virefu ikilinganishwa na nchi za Afrika Mashariki.
Msimbe alieleza kuwa wakati mwanablogu wa Tanzania
analazimika kulipia zaidi ya shilingi 500,000 hadi 1,000,000 kama ada ya maombi
na leseni, nchini Kenya hakuna hitaji la leseni ya gharama hiyo, na nchini
Uganda ada ni rafiki (Tsh 60,000 - 100,000).
Alisisitiza kuwa mfumo wa sasa unamfanya mwanablogu wa
Kitanzania kutumia mtaji wake kulipia 'karatasi' za Serikali badala ya kununua
vifaa bora kama kamera na maikrofoni, jambo linalopunguza uwezo wa kushindana
kimataifa.
Pamoja TCRA kuzungumzia suala la ada na leseni Katibu Mkuu
wa Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amebainisha
dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuachana na mfumo wa kutumia
adhabu dhidi ya wanahabari wa mtandaoni na badala yake kuanza kuwalea kupitia
uwezeshaji wa kiuchumi.
Msigwa katika kikao hicho pia alitangaza kuwa Serikali
inakusudia kuwa na mfuko unaolenga kuwawezesha wanablogu na waandishi wa
mtandaoni kumudu kumiliki vitendea kazi
vya kisasa na kukuza taaluma yao.
Msigwa alifafanua kuwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ni kuhakikisha waandishi wa mitandaoni na mabloga ambao wengi waio ni
Gen Z wanatambuliwa kama washirika muhimu wa maendeleo, na si watu wa kuandamwa
na faini pekee.
Aidha, katika kukabiliana na changamoto za kodi
zinazowakabili mabloga, Msigwa aliahidi kuwa Serikali itakutana na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua kero za kodi kubwa ambazo hazilingani na
kipato cha waandishi. Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha blogu zinatambuliwa
kama biashara ndogo (SMEs) zinazochangia pato la taifa kupitia utalii na uwekezaji,
badala ya kuzitazama kama vyombo vikubwa vya habari vyenye uwezo mkubwa wa
kifedha.

0 Maoni