Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA, Mlage Yussuf Kabange amefungua rasmi kikao kazi cha Menejimenti ya TAWA kilichofanyika Disemba 13,2025, katika ukumbi wa Malaika, jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho
kilichojumuisha Makamishna Wasaidizi Waandamizi, Makamanda wa Kanda na Wakuu wa
Vituo vyote vya TAWA, Kamishna Kabange amesema lengo kubwa la kikao hiki ni
kuboresha utendaji kazi ili kufikia malengo ya Mamlaka.
Kamishna Kabange ameibainisha kuwa kikao kazi hiki
kitajikita katika vipaumbele mbalimbali vitakavyoboresha maeneo ya utendaji
kazi wa TAWA yakiwemo maeneo ya ulinzi na usimamizi wa wanyamapori, ukusanyaji
wa mapato, migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ujenzi wa miundombinu katika
hifadhi pamoja na kuboresha mazingira ya kazi hususan kwenye maeneo ambako
askari wanafanya kazi.
Sambamba na hilo, Kamishna Kabange amewasisitiza
Makamishna Wasaidizi Waandamizi na Makamanda wa Kanda kuhakikisha kuwa
utekelezaji wa majukumu unazingatia utu, sheria na haki bila upendeleo wowote.
Awali, akimkaribisha Kamishna wa Uhifadhi, Naibu
Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Kurugenzi ya Huduma za Shirika, Maarufu
Thabit Mkwaya amesema katika kikao kazi hiki viongozi wa Menejimenti watapata
fursa ya kupitishwa katika mawasilisho mbalimbali yanayolenga kujenga uwezo wa
kiutendaji, kuongeza ubunifu, kujitathmini, kubadili mitazamo na fikira za
viongozi katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Kamishna Maarufu ameongeza kuwa miongoni mwa
mawasilisho hayo ni tathmini ya mpango mkakati wa Mamlaka (2021/22-2025/26) na
maandalizi ya mpango mkakati mpya (2026/27-2030/31), Uongozi wa Kimkakati na
Akili Hisia, Itifaki na Adili kwa viongozi, Afya ya Akili pamoja na Elimu ya
Fedha na Uwekezaji.
Na. Joyce Ndunguru- Mwanza



0 Maoni