AFISA Madini
Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Mayigi Makolobela, amesema mkoa huo umeendelea kufanya
vizuri katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na Sekta ya Madini, ambapo
makusanyo ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 yamevuka malengo kwa
kufikia zaidi ya asilimia 103 ya lengo lililowekwa kwa kipindi husika.
Akizungumza
mkoani Simiyu, Makolobela amesema kwa mwaka wa fedha uliopita, ofisi yake
ilipewa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 4, lakini walifanikiwa kukusanya
zaidi ya Shilingi bilioni 4.5.
“Kwa mwaka huu wa fedha tumewekewa lengo la
kukusanya Shilingi bilioni 4.76, na hadi kufikia robo ya kwanza tayari
tumekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 1.23, sawa na asilimia 103 ya lengo la
robo mwaka,” amesema Makolobela.
Ameongeza
kuwa tangu kuanza kwa Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu
Hassan, makusanyo ya madini kupitia wachimbaji wadogo mkoani humo yamefikia
zaidi ya Shilingi bilioni 17, hatua inayodhihirisha ukuaji na uimara wa sekta
hiyo katika Mkoa wa Simiyu.
Aidha,
Makolobela amesema Simiyu ni miongoni mwa mikoa yenye utajiri mkubwa wa madini
mbalimbali ikiwemo dhahabu, shaba, madini ya ujenzi, vito aina ya Amethyst na
Nikeli yanayopatikana katika wilaya za Bariadi na Busega.
Hata hivyo,
amebainisha kuwa tafiti za kina bado hazijafanyika ipasavyo katika maeneo yote
ya mkoa huo, jambo linaloweza kusababisha baadhi ya maeneo yenye rasilimali
kutobainika mapema.
“Kama Mkoa
huu utafanyiwa utafiti wa kina, kuna uwezekano mkubwa wa kugundulika mashapo
mengine, hususan madini ya metali yanayoweza kuchimbwa kwa kiwango cha kati na
kikubwa, hivyo kuinufaisha Serikali na wananchi kwa ujumla,” amesema
Makolobela.
Katika hatua
nyingine, ameeleza kuwa Mkoa wa Simiyu una vituo vitano vya ununuzi wa madini
pamoja na Soko Kuu la Madini lililopo Bariadi Mjini, ambapo shughuli kuu za
biashara ya madini zinafanyika kwa ufanisi mkubwa.



0 Maoni