MKOA wa Mara
umeweka rekodi mpya katika uzalishaji wa madini baada ya kuzalisha dhahabu
yenye uzito wa tani 67.41, ikiwa na thamani ya Shilingi Trilioni 8.881 katika
kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2021 hadi Oktoba 2025.
Akizungumza
kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Afisa Mazingira, Byalugaba
Chakupewa, hivi karibuni alisema mauzo ya dhahabu hiyo yamechangia mapato ya
Serikali zaidi ya Shilingi Bilioni 605.86 kupitia mrabaha, ada za ukaguzi na
tozo mbalimbali.
Aidha,
Chakupewa alisema kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini mkoani Mara imekusanya
maduhuli ya Shilingi Bilioni 78.7 katika robo ya kwanza ya mwaka, sawa na
asilimia 37.48 ya lengo la mwaka la Shilingi Bilioni 210.3.
Kwa mujibu
wake, ofisi hiyo pia imetoa leseni 2,478 za shughuli za madini, hatua
iliyosaidia kuongeza ajira, kuchochea uwekezaji na kuimarisha mapato ya
halmashauri.
Alibainisha
kuwa mafanikio hayo yanatokana na usimamizi madhubuti wa sekta hiyo na
mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo yameufanya Mkoa wa Mara
kuendelea kuwa miongoni mwa vinara wa uzalishaji wa madini nchini.




0 Maoni