Wataalam
wa Maendeleo ya Jamii wana jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa jamii
inaishi katika maadili ikiwemo
kuzingatia mila na desturi za kitanzania zinazofaa.
Hayo
yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Makundi Maalum Felister Mdemu alipotembelea Chuo cha Maendeleo ya Jamii-Ruaha jana
6 Oktoba 16, 2025 mkoani Iringa.
Felister
ameeleza kuwa nidhamu katika jamii haipo tena na wimbi la mmomonyoko wa maadili
limekua kubwa kwani vijana hawana hofu ya kutumia lugha zisizofaa hadharani na
kwenye mitandao ya kijamii hata kwa watu waliowazidi umri.
“Jamii
zetu sasa hivi zinakwenda kinyume na maadili ya kitanzania kwani tunaona kwenye
mitandao ya kijamii vijana wakitukana ovyo bila kujali na hiki ni kiashiria
kuwa kuna shida sehemu hivyo basi
Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wana jukumu la kufanya tafiti na kuja na
majibu yenye suluhisho ili kutokomeza mmonyoko wa maadili,” amesema Felister.
Vilevile
Felister amekipongeza Chuo cha Maendeleo ya Jamii-Ruaha kwa kazi nzuri
inayokifanya kwa kuwainua mabinti wa kike na kuwajengea uwezo wa kujikomboa
kiuchumi ikiwemo kushona cherehani na stadi nyingine za maisha.
“Mabinti
hawa wanachukua kozi ya miezi sita na baada ya muda huo wanaenda mtaani
kujitegemea hivyo basi nimefurahishwa na juhudi zao na nimetoa ahadi kuwa
Wizara itawaongezea cherehani mbili ili waweze kuongeza nguvu,” amesema
Felister.
Naye
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo Ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Patrick Golwike amesema Serikali inapambana
kuhakikisha Vyuo hivyo vya kati vinatoa mafunzo stahiki kwa wanafunzi na
kunufaisha jamii za sehemu husika kupitia afua mbalimbali hivyo itaendelea
kuvisimamia na kuvijengea uwezo.
Halikadhalika,
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii-Ruaha Godfrey Mafungu ametoa pongezi kwa
Serikali hususani Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum kwa kutenga muda wao kukagua
mafunzo na miradi inayotekelezwa na Chuo hicho ili kuweza kuwajengea
uwezo zaidi na kuhakikisha mambo yote yako sawa.
Na.
Witness Masalu - WMJJWM - Iringa



0 Maoni