Vijana wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamekataa
kushiriki maandamano yaliyopangwa kufanyika siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, na
badala yake wameahidi kushiriki kikamilifu kupiga kura kwa amani, wakisisitiza
umuhimu wa kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Makundi yaliyoshiriki kutoa tamko hilo ni pamoja na
waendesha bodaboda na bajaji, wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga,
mamalishe, walinzi wa jadi (Sungusungu) pamoja na wachimbaji wadogo wa madini.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika viwanja vya
Magereza, Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Mwime Ilindi, Mohamed
Juma, alisema vijana wa Kahama wamejipanga kushiriki uchaguzi kwa amani na
hawako tayari kujiingiza kwenye maandamano yoyote.
“Siku ya uchaguzi tutasitisha shughuli za uzalishaji
ili tukapige kura, ni haki yetu ya kikatiba hatutaki kuona uchaguzi unageuzwa
uwanja wa vurugu, mwaka huu tumeamua kuwa mfano wa kuigwa kwa kutanguliza
maslahi ya Taifa mbele,” amesema Juma.
Naye Mwenyekiti wa waendesha pikipiki na bajaji mkoa
wa Shinyanga, Idisam Mapande, amesema vijana wanatambua kuwa wapo watu
wanaohamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii huku wakiwa nje ya nchi,
hivyo hawana nia njema na Tanzania.
“Tumeamua hatutashiriki maandamano yoyote siku ya
uchaguzi, Tunataka kuonyesha kwamba vijana wa nchi hii ni wazalendo na wanajali
amani ya nchi yao, Maandamano yanaweza kutoa mwanya kwa watu wasiopenda amani
kuchochea vurugu, jambo ambalo halitavumiliwa,” amesema Mapande.
Kwa upande wake, msemaji wa walinzi wa jadi (Sungusungu),
Wiliamu Mondi, amesema wanatambua thamani ya amani ambayo ni tunu waliyoachiwa
na waasisi wa Taifa, na hivyo wataendelea kuilinda kwa nguvu zote.
“Tunapenda kumhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa
hakutakuwa na maandamano, Twendeni tukachague wagombea wetu kwa amani na
tupinge uchochezi,” amesema Mondi.
Mzee wa jadi, Ukuku, amewasihi vijana kutoshiriki
vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi, akibainisha kuwa amani
ndiyo imemwezesha kufika umri wa miaka 72.
“Amani iliyopo sasa nchini Tanzania ndiyo
imeniwezesha kuishi miaka yote hii. Vijana mna ushawishi mkubwa, tumieni nguvu
zenu kulinda amani ya nchi yetu,” amesisitiza Mzee Ukuku.
Mwenyekiti wa machinga wa Wilaya ya Kahama, Idrisa
Kayombo, naye ameongeza kuwa vijana wa kundi hilo wamepata fursa nyingi kupitia
mikopo na mazingira bora ya biashara chini ya serikali ya awamu ya sita, hivyo
hawana sababu ya kushiriki maandamano.
“Samia ametuwezesha kupata mikopo na kufanya
biashara bila usumbufu, Tutaenda kupiga kura kwa amani, siyo kuandamana,”amesema
Idrisa.
Aidha, wachimbaji wadogo wameeleza kuwa serikali
imewapa leseni na kupunguza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo, hivyo
wanathamini maendeleo yaliyopatikana na hawako tayari kuyaharibu kwa kushiriki
vurugu.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amewapongeza
vijana hao kwa uamuzi wa busara, akisema serikali inathamini mchango wao katika
kulinda amani na kuimarisha demokrasia.
“Nawapongeza sana vijana, bodaboda, machinga,
wachimbaji wadogo na wazee wa jadi kwa hatua hii ya kuonyesha ukomavu wa
kisiasa, Wilaya ya Kahama iko salama kabisa, na yeyote atakayevuruga amani
atashughulikiwa kisheria,” amesema Nkinda.
Vijana hao wameahidi kushiriki uchaguzi huo kwa
amani, huku wakisisitiza kuwa Tanzania haina utamaduni wa maandamano bali ni
nchi inayojivunia umoja, upendo na utulivu.
Na. Neema Nkumbi - Kahama



0 Maoni