Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema Serikali inajipanga kuufanya uwanja wa ndege mpya wa Msalato kuwa kituo cha huduma za usafiri wa anga kwa mizigo na abiria katika eneo la nchi za maziwa makuu ili kuchochea maendeleo.
Akizungumza
wakati wa kuukaribisha ujumbe wa wataalam kutoka Tanzania kwenye Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Arlanda jijini Stockholm, Sweden, Balozi Matinyi aliwaambia
watendaji wa kampuni ya Avia Solutions Group walioongozwa na Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Biashara, Magnus Söderberg na Mkuu wa Miradi, Andrej Boicisin,
kwamba Serikali ya Tanzania inataka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato uwe
kitovu cha uwekezaji na biashara ya kimataifa kati ya nchi za eneo hili la
Afrika na dunia.
Balozi
Matinyi aliongeza kuwa nia zaidi ya Serikali ni kuwapatia huduma zenye viwango
vya kimataifa wasafirishaji wa bidhaa za matunda, mbogamboga na maua kutoka
Tanzania na nchi jirani kwenda kwenye soko la kimataifa.
Ujumbe wa
Tanzania unaomjumuisha Mkurugenzi wa Miundombinu ya Usafirishaji kutoka Wizara
ya Uchukuzi, Mhandisi Shomari Shomari; Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Msalato, Clemence Jingu na Mwanasheria wa Mamlaka ya Uwekezaji na
Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Shani Mayosa, upo nchini Sweden na baadaye
Lithuania ili kujionea teknolojia na uendeshaji wa viwanja vya ndege unaofanywa
na kampuni hii ambayo ni moja kati ya kubwa barani Ulaya.
Kampuni
ya Avia Solutions Group yenye uzoefu wa miaka 50 na inayomiliki ndege za kukodi
221, inasimamia viwanja vya ndege 15 katika nchi za Sweden, Norway, Finland na
Denmark na vingine zaidi barani Ulaya na katika mabara mengine.
Ujenzi wa
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma umefikia asilimia 94 kwa
miundombinu na asilimia 62 kwa majengo. Inatarajiwa ujenzi huu utakapokamilika
utawezesha safari za ndani na za kimataifa na kuongezea fursa za biashara,
uwekezaji na utalii kwa kuufanya uwanja huo kuwa kitovu cha safari za anga kwa
ukanda wa Maziwa Makuu.
Balozi wa
Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, akizungumza na Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Biashara wa kampuni ya Avia Solutions Group, Magnus Söderberg,
wakati wa kuukaribisha ujumbe wa Tanzania uliokuja kuona teknolojia na
uendeshaji wa kampuni hiyo katika viwanja vya ndege vya nchi za
Sweden na Lithuania.
Ubalozi
wa Tanzania Stockholm, 13 Oktoba, 2025.


0 Maoni