Hospitali
ya Taifa Muhimbili Mloganzila inaendelea na kambi maalum ya ubingwa bobezi ya
kutengeneza na kurekebisha mishipa ya kuchuja damu kwa wagonjwa wenye
changamoto ya figo, kambi ambayo inaenda sambamba na upandikizaji wa figo kwa
wagonjwa wenye changamoto hizo.
Kwa
mujibu wa Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Daudi Katwana, kambi hiyo inafanywa
na wataalam wa hospitali hiyo kwa kushirikiana na jopo la wataalam kutoka Korea
Kusini linaloongozwa na Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Dkt. Park Kwan Tae
chini ya uratibu wa Taasisi ya Africa Future Foundation (AFF) ya nchini Korea.
“Tulianza
kambi hii siku ya Jumamosi Oktoba 11, 2025, ambapo mpaka sasa tumefanikiwa
kutengeneza na kurekebisha mishipa ya kuchuja damu kwa wagonjwa wapatao 10,
zoezi limeenda vizuri na tutaendelea hadi siku ya Jumanne Oktoba 14, 2025”
ameongeza Dkt. Katwana.
Dkt.
Katwana amebainisha kuwa huduma hizo ni endelevu, na wapo tayari kuendelea
kuhudumia wagonjwa watakaojitokeza hata baada ya kambi hiyo kuisha, hivyo
wasisite kufika katika hospitali hiyo ili kunufaika na huduma hizo.
Hospitali
ya Taifa Muhimbili Mloganzila ndio hospitali pekee hapa nchini inayotoa
matibabu ya ubingwa bobezi ya kupandikiza figo kwa kuvuna figo kutoka kwa
mchangiaji kwa kutumia matundu madogo (Hand Assisted Laparoscopic Donor
Nephrectomy) huduma ambayo hupunguza muda wa mchangiaji kukaa hospitalini,
kutokuwa na makovu makubwa na kupona haraka.

0 Maoni