Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa, Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani 2025 unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025 ni halali kwakuwa
umefuata misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za Uchaguzi.
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ameyasema hayo katika Mkutano na Vyombo vya Habari uliofanyika Ofisini
kwake Mtumba Jijini Dodoma, tarehe 28 Oktoba, 2025.
Akizungumza katika
mkutano huo Mhe. Johari amesema kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni kwa mujibu wa masharti
yaliyowekwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Aidha, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ameeleza kuwa, ni haki ya kila Mtanzania aliyetimiza umri wa miaka
18 kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kama ilivyoainishwa
katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ibara ya 5(1) ya
Katiba yetu inatoa haki kwa kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka
kumi na minane kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na Wananchi.”
Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha wananchi kuwa kutokana na masharti
yaliyowekwa na wananchi katika katiba, Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani,
unafanyika kila baada ya miaka mitano kama ilivyoanishwa katika Ibara za 42(2)
na 65(1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kifungu
cha 56(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka
2024.
“Naomba mfikishe ujumbe
kwa wananchi wote kuwa, miaka mitano imeshamalizika kwa mujibu wa Katiba na
sasa uchaguzi wa kesho upo kwa mujibu wa Katiba hiyo na kwamba wagombea wote wa
nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani nchi nzima wamepatikana kwa mujibu wa Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo uchaguzi huu ni HALALI.” Amesema Mhe.
Johari.
Vilevile, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ametumia Mkutano huo kutoa onyo kwa wote wanaopanga kuvuruga
au kushawishi wananchi kutokushiriki uchaguzi ni kosa kisheria kwa mujibu wa
Kifungu cha 129 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.




0 Maoni