Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Ruvuma umeendelea kunufaika na
uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya barabara, hatua inayochochea
maendeleo ya kiuchumi, kilimo, na uhifadhi wa mazingira.
Meneja wa
TARURA mkoa wa Ruvuma, Mhandisi
Silvester Chinengo, amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, mkoa huo unatekeleza
miradi ya maendeleo yenye bajeti ya shilingi bilioni 22, ikiwa ni ongezeko
kubwa kutoka bilioni 7 za awali.
“Kwa
sasa, TARURA Ruvuma inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita
7,147, ambapo kilomita 133.69 ni za lami, 1,651.8 ni za changarawe, na 5,360.6
ni za udongo. Takribani asilimia 70 ya barabara hizo zinapitika msimu wote,
jambo ambalo limeleta mabadiliko chanya kwa wakulima na wafanyabiashara wa mkoa
huo”.
“Barabara
hizi zimekuwa mkombozi kwa wakulima. Mazao kama mahindi na kahawa sasa yanafika
sokoni kwa wakati, bila kuharibika njiani na hivyo kuongeza uchumi kwa
wakulima", amesema Mhandisi Chinengo.
Aidha,
Meneja huyo amesema TARURA imefanya manunuzi ya mikataba 43 yenye thamani ya
shilingi bilioni 12.1, na iko katika hatua za mwisho za kusaini mikataba hiyo.
Ameongeza
kusema kwamba kwa mwaka uliopita pekee, zaidi ya kilomita 3 za barabara za lami
zimejengwa, na taa za barabarani zimewekwa ili kuongeza usalama na mwonekano wa
mji kwa usiku.
“Kwa
sasa, kila barabara inayojengwa inaambatana na uwekaji wa taa hatua inayoongeza
usalama na kuchochea shughuli za kiuchumi hasa nyakati za usiku.
Katika
kulinda mazingira, Mhandisi Chinengo amewataka wananchi kutotupa taka kwenye
mitaro ya maji na kushiriki katika utunzaji wa miundombinu.
“Serikali
imewekeza fedha nyingi ni jukumu letu kuhakikisha barabara hizi zinadumu kwa
muda mrefu kwa kuepuka uharibifu wa makusudi,” amesisitiza.
Naye, Bi.
Eva Ndomba mkazi wa Makambi amesema awali barabara zilikuwa na nyasi, vumbi na
hata pikipiki zilikuwa zinapata changamoto kupita ila wanaishukuru Serikali kwa
ujenzi wa barabara za lami kwani wanapita vizuri na uwekaji wa taa umewasaidia
kwa sasa wanafanya biashara hata usiku.
Wakati
huo huo, Bw. Ally Musa ambaye ni mkazi wa Makambi amesema wanashukuru kwa
ujenzi wa barabara ya lami awali hususan kipindi cha masika walikuwa wakipita
vichochoroni lakini sasa wanakatiza kwenye barabara na uwekaji wa taa wao kama
vijana zimewasaidia kufanya shughuli zao hadi usiku.




0 Maoni