Balozi wa
Tanzania nchini Sweden, Mhe. Balozi Mobhare Matinyi, aliongoza ujumbe wa
Tanzania katika Mkutano wa Biashara kati ya nchi za Nordic na Afrika
uliofanyika jijini Oslo, Norway.
Akifungua
mkutano huo Oktoba 9, 2025, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Andreas
Motzfeldt Kravik, alieleza kuwa ni muhimu nchi za Nordic na Afrika ziwe na sera
rafiki za pamoja za kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha ushirikiano
kati ya sekta za umma na binafsi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, na
kwamba bara la Afrika linabeba mustakabali wa dunia.
Washiriki
wa mkutano huo unaofanyika kila mwaka walitoka sekta binafsi, jumuiya za
wafanyabiashara, viongozi wa serikali, wanadiplomasia na washiriki wengine
kutoka asasi za nchi mbalimbali duniani ikiwemo Marekani. Kaulimbiu ya mkutano
huo ilijikita katika kuhamasisha biashara, matumizi ya nishati safi, na
ushirikiano wa kuimarisha miundombinu kati ya nchi za Nordic na Afrika.
Ujumbe wa
Tanzania chini ya Balozi Matinyi ulimjumuisha pia Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama
cha Wakulima wa Maua, Matunda na Mbogamboga (TAHA), Jacqueline Mkindi, na
ulitumia fursa hiyo kutafuta masoko mapya ya bidhaa za Tanzania, hususan
kahawa, chai, korosho, vitunguu, viungo vya vyakula, maua na matunda.
Katika
matumizi ya nishati safi, Balozi Matinyi alifanya mazungumzo ya awali na
kampuni za nishati za SCATEC iliyowakilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Terje
Pilskog; RENERGY iliyowakilishwa na Afisa Uendeshaji Mkuu, Mikkel Hansen; na
CAMBI iliyowakilishwa na Meneja wa Mauzo wa Kanda ya Afrika, Gary Brown.
Ujumbe wa
Tanzania ulijikita pia kutafuta fursa za ushirikiano za kupunguza utoaji wa
hewa ya ukaa na majitaka kwa kuendeleza teknolojia bunifu za nishati safi,
ambazo ni muhimu kwa mabadiliko ya mfumo wa nishati wa Tanzania; pamoja na
fursa za kuendeleza mnyororo wa thamani kwenye sekta ya madini kupitia ujenzi
wa miundombinu imara na rafiki kwa wachimbaji wadogo.
Ubalozi
wa Tanzania, Stockholm, Sweden


0 Maoni