Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA), Mhandisi Victor Seff amesema katika kipindi cha miaka minne (4) ya
Serikali ya Awamu ya Sita, Wakala umekamilisha ujenzi wa miradi mikubwa ya
miundombinu ya barabara za Wilaya yenye thamani ya Shilingi Bilioni 262.46 huku
miradi yenye thamani ya Shillingi Bilioni 40.49 ikiwa katika hatua mbalimbali
za utekelezaji na miradi yote ikikamilika itakuwa na thamani ya Shilingi
Bilioni 302.95.
Mhandisi Seff amesema mafanikio hayo yametokana na ongezeko
la bajeti lililofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa TARURA ambapo awali
walikuwa wakipokea bajeti ya Shilingi Bilioni 275 kwa mwaka lakini baada ya
Serikali ya Awamu ya Sita kuona kazi kubwa ya TARURA bajeti iliongezeka kutoka
Bilioni 275 kwa mwaka hadi kufikia Shilingi Trilioni 1.1 sawa na ongezeko la
asilimia 230.
“Baadhi ya miradi iliyokamilika ni ujenzi wa barabara za
lami Kilomita 58.5 katika mji wa Serikali Mtumba-Dodoma, daraja la Berega mita
140 wilayani Kilosa-Morogoro, daraja la Mbwemkuru mita 75 wilayani
Ruangwa-Lindi, barabara ya lami Visiga-Zegereni Kilomita 12.5 wilayani
Kibaha-Pwani na barabara ya lami Kilomita 5.1 katika eneo la viwanda Dodoma,” amesema.
Ameeleza kuwa, Wakala umeendelea na usimamizi madhubuti wa
miradi ya wadau wa maendeleo ya Benki ya Dunia na Umoja wa Nchi za Ulaya.
Miradi hiyo ni Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP 2) wenye thamani ya
Shilingi Bilioni 1,136.172 {US$ 438 milioni}, Uendelezaji wa Bonde la Mto
Msimbazi (MBD) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 608.4 {US$ 260 milioni) na
Uboreshaji wa Miji 45 (TACTIC) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 959.4 {US$ 410
milioni}.
Miradi mingine ni uboreshaji wa barabara za vijijini na fursa
za kijamii na kiuchumi kwenye maeneo yenye fursa za kilimo (RISE) wenye thamani
ya Shilingi Bilioni 811.65 {US$ 350 milioni}) na Ujenzi wa barabara kwenye
maeneo ya kilimo cha mazao ya Kahawa, Chai, matunda na mbogambaga
(Agri-connect) wenye thamani ya Shilingi Bilioni 138.528 {EUR 48 milioni}.
“Miradi hii ikikamilika itagharimu takribani Shilingi
Trilioni 3.68 na hadi sasa utekelezaji wa jumla umefikia asilimia 40 na miradi
yote inategemewa kukamilika ifikapo mwezi Aprili 2030. Miradi hii ikikamilika
jumla ya Kilomita 1,242.52 za barabara za lami, Kilomita 151 za mifereji,
masoko 56 na stendi za mabasi 39 vitakuwa vimejengwa,” ameongeza.
Aidha, Mhandisi Seff amesema Wakala umetekeleza miradi ya
ujenzi na matengenezo ya barabara za Wilaya kwa kuzingatia sera za ushiriki,
ushirikishwaji na uwezeshaji wa jamii kiuchumi ambapo asilimia 99.2 ya zabuni
za ujenzi na matengenezo ya barabara za vijijini na mijini zimekuwa zikitolewa
kwa makandarasi wazawa kila mwaka huku asilimia 30 ya bajeti ya Mfuko wa Barabara
hutumika kutoa zabuni kwa makundi maalumu kila mwaka.
“Jumla ya vikundi 344 vya wananchi vimeshiriki kwenye kazi
za matengenezo ya barabara na hadi kufikia Julai, 2025 ajira 173,760 zilitolewa
kwa wananchi kwenye miradi ya ujenzi wa barabara,” amesema.
Vilevile, ameongeza kuwa Wakala kwa kushirikiana na Taasisi
ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (Economic and Social Research
Foundation-ESRF), umefanya tathmini ya matokeo ya uboreshaji wa barabara za
vijijini na ufikiwaji wake kwa wananchi, mwaka 2025. Tathmini hiyo imeonesha
matokeo makubwa yaliyopatikana baada uboreshaji wa mtandao wa barabara za
Wilaya.
“Tathmini imeonesha, muda wa usafiri na usafirishaji kwenda
kwenye huduma za kijamii na kiuchumi kama masoko na hospitali umepungua kwa
dakika 17.5, gharama za usafiri na usafirishaji zimepungua kwa asilimia 75.3,
hali ya upatikanaji wa usafiri na usafirishaji imefikia asilimia 86
ikilinganishwa na asilimia 20 kwa barabara ambazo hazijaboreshwa na endapo
barabara zikiboreshwa kwa kiwango cha lami au changarawe hali ya usafiri
inaongezeka kwa takribani asilimia 66 na upotevu wa mazao umepungua kwa
asilimia 72.5 kutokana na uboreshaji wa barabara vijijini”.
Ameendelea kufafanua “kiwango cha ufikiwaji wa mtandao wa
barabara za Vijijini unaopitika majira yote ya mwaka kimeongezeka kutoka
asilimia 24.6 mwaka 2016 hadi asilimia 61.0 mwaka 2025, hii inaonesha kwamba
sehemu kubwa ya wakazi wa vijijini wana pata huduma za usafiri na usafirishaji
jambo ambalo ni muhimu kupunguza umasikini, upatikanaji wa huduma na ukuaji wa
Uchumi”.
Katika hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto za
mitaji kwa Makandarasi Wazawa katika kutekeleza kazi za barabara za Wilaya,
Mhandisi Seff ameeleza kuwa Wakala kwa kushirikiana na Benki ya CRDB imeratibu
uanzishwaji wa Hati Fungani ya Miundombinu iitwayo “SAMIA INFRASTRUCTURE BOND”
kwa lengo la kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 150 ili kuwasaidia Wakandarasi
wazawa kupata fursa za mikopo ya fedha na dhamana za kazi kwa gharama nafuu.
“Kiasi cha Shilingi Bilioni 323.09 zimekusanywa ikiwa ni asilimia 215.4 ya lengo lililowekwa ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 223.8 kimeombwa na Wakandarasi Wazawa wapatao 276 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za mikataba ya matengenezo na ujenzi wa barabara”.



0 Maoni