Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),
limezindua rasmi Programu Tumizi "App" yake Leo Oktoba 08, 2025
katika viwanja vya Hifadhi ya Taifa Mikumi ikilenga kupanua wigo wa utalii kwa
kurahisisha upatikanaji wa taarifa za vivutio vya hifadhi zote za Taifa nchini.
Akizindua Programu hiyo Tumizi Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas ambaye ni Mgeni rasmi amepongeza
juhudi hizo za kutangaza utalii kupitia teknolojia hasa ile inayopatikana katika simu janja ya
kiganjani huku akitoa Takwimu za watumiaji wa simu janja za viganjani pamoja na
intaneti duniani.
"Dunia ina jumla ya watu Bilioni nane Watu
zaidi ya Bilioni tano wanatumia simu za mkononi na kati ya watumiaji hao asilimia
87% wana simu janja. Na watu Bilioni 5.7 ni watumiaji wa intaneti duniani.
Hivyo basi "App" hii inakuja wakati muhimu sana leo kwani inaenda
kutatua changamoto yetu kubwa ya kujitangaza katika soko la utalii duniani.
Programu tumizi hii itaturahisishia mambo mengi, inatusaidia kujua fursa za
uwekezaji zinazopatikana katika hifadhi zote za Taifa nchini, kadhalika taarifa
rasmi za hifadhi husika bila ukakasi".
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Mkuu wa
Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara amesema kuwa Programu hiyo tumizi
"App" itaongeza ufanisi katika shughuli za Utalii na Uhifadhi na
kuipongeza Menejimenti ya Shirika kwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya
TEHAMA.
"Nimekuwa nikiwaambia hakuna kinachoshindikana
ni kudiriki na uthubutu. Niwapongeze Menejimenti ya TANAPA kwa ubunifu huu wa
Programu Tumizi "App" hii ya "TANAPA GO" itaimarisha
utendaji wa Shirika na kuwa wa haraka na wenye ufanisi mkubwa kwani huduma
pamoja na taarifa mbalimbali zitawafika wageni wa ndani na nje ya nchi. Kazi kubwa mmeifanya
kwa pokeeni pongezi za Bodi ya Wadhamini".
Awali, akitoa neno la Utangulizi Naibu Kamishna wa
Uhifadhi Maendeleo ya Biashara TANAPA Masana Mwishawa ameeleza kuwa Programu
Tumizi hiyo ni daraja kubwa katika kuongeza na
kukuza maendeleo ya sekta ya uhifadhi na Utalii. App hii (TANAPA
GO) itachangia kwa upana upatikanaji wa
taarifa za Hifadhi kwa wepesi kwa watalii wote wanaotembelea au wanaopanga
kutembelea Hifadhi za Taifa nchini.
Na. Calvin Katera - Mikumi




0 Maoni