Mgombea urais wa Tanzania
kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
ameainisha mikakati ya kuinua maendeleo ya Mkoa wa Mwanza akitaja maeneo matatu
yatakayochochea uchumi na biashara katika miaka mitano ijayo.
Dkt. Samia ameyasema hayo Jumatano Oktoba 8, 2025
alipohutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika mkutano mkubwa wa
kampeni uliofanyika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni ujenzi wa Reli ya
Kisasa (SGR) kipande cha Mwanza hadi Isaka chenye urefu wa kilometa 314 ambacho
ujenzi wake umefikia asilimia 63 na una thamani ya Shilingi trilioni tatu.
Amebainisha kuwa mkoa huo utakuwa na vituo vitano
vya kushusha na kupakia abiria na mizigo ambapo vituo hivyo vitachochea
shughuli mbalimbali za kiuchumi kama malazi kwa kujengwa mahoteli.Amewahimiza
wakazi wa Mwanza kuchangamkia fursa hizo za kiuchumi kwa kuwekeza mkoani humo.
“Stesheni
tano ndani ya Mkoa wa Mwanza ni fursa kubwa ya kiuchumi, ni ajira kwa vijana
wetu na kwa watu wa Mwanza kwa ujumla,” amesema Dkt. Samia.
Mbali ya
ujenzi wa mahoteli na maduka katika vituo hivyo, amesema serikali itajenga
maghala ya kuhifadhia bidhaa ambazo zitatakiwa kusafirishwa kwenda maeneo
mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam au nje ya nchi.
Dkt. Samia ameeleza kuwa eneo la Fela kuna bandari
kavu ambayo ni fursa nyingine ya kiuchumi na ajira kwa vijana, na kufafanua
kuwa reli hiyo itakapokamilika kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza itarahisisha
usafiri na usafirishaji pamoja na biashara kwani itatumia muda mchache wa
takriban saa nane.
Mgombea huyo amebainisha pia kuwa gharama za
usafirishaji na bei zitashuka hivyo itasaidia katika kupunguza mfumuko wa bei
na kupunguza kiwango cha umaskini kwani bidhaa zitauzwa kwa bei nafuu.
Dkt. Samia ambaye kwa Mwanza anasema ni nyumbani
kwake na anafahamika pia kwa jina la Chifu Hangaya, amelitaja eneo la pili kuwa
ni uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miradi ya Ziwa Victoria.
Miradi hiyo ni pamoja na ukarabati wa meli ya mizigo
ya MV Umoja kwa Shilingi bilioni 19.8 ambayo inafanya kazi na inabeba tani
1,200 za mizigo kwenda Uganda ikifungua masoko mapya kwa wakulima na
wafanyabiashara.
“Pia ukiangalia ziwani unaona meli mpya ya kisasa ya
MV Mwanza, fahari ya Ziwa Victoria ambayo imewekezwa zaidi ya Shilingi bilioni
120 na sasa imekamilika kwa asilimia 98 na wiki mbili zilizopita ilifanya
majaribio ndani ya ziwa na wanamalizia asilimia mbili ili meli ianze safari
zake,” alieleza Dkt. Samia aliyefanya mikutano minne mikubwa katika mkoa huo
kitovu cha biashara na uchumi Kanda ya Ziwa.
Amesema meli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria
1,200 na tani 400 za mizigo na gari 20 pamoja na malori makubwa matatu
yanayovuka kwenda nchi nyingine kwa wakati mmoja, akisema “hiyo sio meli tu,
bali ni alama ya heshima na uwezo wetu wa kujiletea maendeleo kwa fedha zetu
wenyewe”.
Ametaja pia upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini
kwa gharama ya Shilingi bilioni 18.6,ukarabati na ujenzi wa vivuko vipya vitano
vitakavyochochea shughuli za kiuchumi, na pia kupeleka boti za doria, na za
kubeba wagonjwa katika Kisiwa cha Ukerewe.
Kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza amesema
kinaenda kukamilika na kuwa cha kimataifa ili kurahisisha njia ya watalii
kwenda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na hivyo kukuza sekta ya utalii.
Kwenye kilimo, Dkt. Samia amewapa faraja wakulima wa
pamba kwa kusema serikali imesambaza mbegu na dawa bure na imeajiri maofisa
ugani 700 kwa kushirikiana na sekta binafsi kukuza zao hilo.
Aidha, amesema tayari matrekta 700 yameagizwa na 350
yameshawasili nchini na yatagawiwa kwa wakulima ambayo watayakodi kwa nusu bei,
na yatawekwa katika vituo vya zana za kilimo katika kanda.
Kwenye viwanda, ametaja hatua za kufufua viwanda vya
kusafisha pamba pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza na kukijengea
uwezo ili kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwamo zinazotumika hospitalini.
Ametangaza neema katika matumizi ya maji nchini
akisema mbali ya kutumika kwa wananchi yakiwamo kutoka Ziwa Victoria, baada ya
kukamilika kwa Gridi ya Taifa ya Maji, kinachofuata ni kuyatumia maji hayo kwa
umwagiliaji ili yalipe fedha zinazotumika sasa kupeleka maji ya kunywa kwa
wananchi.
“Kwa hiyo tumeamua maji kutoka katika maziwa yetu
tutayatumia katika kujenga Gridi ya Maji Kitaifa na kuyatumia kwa kilimo cha
umwagiliaji ili njiani yanapopita wananchi wa Tanzania wayatumie kwa kumwagilia
mashamba na tupate mavuno makubwa zaidi,” alieleza.
Amesema wanafanya hivyo kwa sababu serikali ya CCM
ina ajenda ya kukuza sekta ya kilimo ambayo kwa sasa inakua kwa asilimia tano
lakini lengo ni kuifanya sekta hiyo ifikapo mwaka 2030 ikue kwa asilimia 10.
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt.
Asha-Rose Migiro amempokea mwanachama mpya wa CCM kutoka Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) ambaye alikuwa ni Katibu wa Mkoa wa Mwanza, Boniface
Mkobe aliyesema amehama kwa sababu Chadema imekuwa ikihamasisha vurugu na chuki
na kufarakanisha wananchi.
Na. Aboubakary Liongo - Mkuu wa Kitengo cha Habari
na Mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM
0 Maoni