Serikali
kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa mwaka wa fedha
2025/2026 imetenga jumla ya shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya maendelezo ya
miundombinu ya barabara wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Hayo
yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori wakati akielezea uendelezaji
wa miundombinu ya barabara unaofanywa na TARURA wilayani humo.
Amesema
ujenzi wa barabara kupitia Wakala huo umeweza kuwasaidia wananchi kusafirisha
mazao yao pamoja na kuinua uchumi katika halmashauri zote mbili za wilaya ya
Mbinga.
“Wilaya
ya Mbinga ni miongoni mwa kapu la chakula la Taifa kwani kuna uzalishaji mkubwa
wa mazao ya chakula na biashara, mazao mengi ya chakula na biashara yanastawi
kutokana na rutuba ya eneo hili”.
“Tunaishukuru
serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
jinsi ambavyo anavyoendelea kutuletea fedha kupitia TARURA kwa ajili ya
shughuli za uendeshaji wa miundombinu ya barabara na kuboresha mazingira,” ameongeza
Mhe. Makori.
Aidha,
amesema kwamba wilaya ya Mbinga kuna mabonde na milima kama kusingekuwa na
uwekezaji wa Serikali kupitia TARURA hata uzalishaji wa mazao hayo ungekuwa
tabu hususan kwenye kufikia maeneo ya uzalishaji. "Tunaishukuru Serikali
inavyoleta fedha katika eneo la barabara”.
Hata
hivyo, ameitaka TARURA kuendelea kuweka taa za barabarani katika maeneo mengine
ili kupendezesha mji na kusaidia kuleta mazingira mazuri na kuongeza usalama
kwa wananchi.
Pia,
amewataka wananchi kuendelea kutunza barabara na miundombinu mingine ili iweze
kudumu kwa muda mrefu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
“Wananchi
tushirikiane katika kutunza mazingira na barabara kwani ni uwekezaji mkubwa
unafanyika katika maeneo yetu na kaleta ) maendeleo.
Kwa
upande wa TACTIC Mhe. Makori amesema wilaya yake imepata miradi mitatu
ikiwemo ujenzi wa barabara za lami zenye
urefu wa Km. 6 katika Mji wa Mbinga, ujenzi wa stendi mpya ya kisasa katika
kata ya Lusaka pamoja na soko jipya na la kisasa.
“Kumekuwa
na changamoto ya soko kwa muda mrefu kulingana na hadhi ya wilaya yetu hivyo
kuja kwa mradi huu italeta mapinduzi makubwa katika upatikanaji na utoaji wa
huduma kwa wananchi hivyo sisi tumekaa mkao mzuri wa kusubiri matunda mazuri
yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita”.
Wakiongea
kwa nyakati tofauti wakazi wa wilaya ya Mbinga wamefurahia uwekaji wa taa za
barabarani kwani umewaongezea usalama na muda wa kufanya biashara.
Bw.
Adrian Frank mkazi wa kata ya Masumuni amesema TARURA imewasaidia sana kwenye
ujenzi wa miundombinu, kwani biashara zao sasa hivi wateja wanafurahia kwa kuwa
kwa sasa hakuna vumbi ukilinganisha na zamani ambapo kulikuwa na matope na
vumbi.
Ameongeza
kuwa uwekaji wa taa umewasaidia kuondoa uhalifu kutoka Tanki la maji kwenda Mji
Mwema kulikuwa na msitu hivyo kwa kuwekewa taa sasa hivi hawaogopi kutembea
usiku na wanapita muda wowote hata usiku kurudi nyumbani.
Naye, Bi.
Christina Mapunda mkazi wa Mji Mwema ameishukuru Serikali kwa uwekaji wa taa
kwani hivi sasa ile tabia ya uvunjaji wa maduka
wakati wa usiku hakuna tena, pia hivi sasa wanatembea bila uwoga hata
kama ni saa sita usiku mara wanapomaliza kufanya biashara zao.


0 Maoni