WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali
itaendelea kuhakikisha Tanzania inakuwa na nguvukazi yenye ujuzi wa kisasa na
inayoweza kushindana katika soko la ajira la kikanda na kimataifa.
Amesema lengo ni kuhakikisha nguvu kazi hiyo inakuwa
na mchango katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa
ujumla.
Amesema hayo leo Jumamosi (Oktoba 11, 2025) wakati
alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Kongamano la
Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lilizofanyika katika ukumbi wa
Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Mafanikio ya taifa letu katika miaka ijayo
yatategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa watu wake. Msingi wa maendeleo ya taifa
letu ni watu wenye ujuzi, ubunifu, na maadili. Tuweke mbele elimu bora, ujuzi,
ubunifu, na uzalendo kama silaha za kujenga taifa lenye ustawi, amani, na
maendeleo jumuishi.
Amesema kuwa katika kuhakikisha Tanzania inaandaa
nguvu kazi imara imetekeleza mipango mbalimbali ikiwemo kuanzisha Programu za
Elimu ya Ufundi na Ujuzi (VET na TVET) kwa kupanua wigo wa vyuo vya VETA katika
kila Wilaya na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mafunzo ya vitendo.
“Pia, Serikali imeanzisha Programu ya Taifa ya
Maendeleo ya Ujuzi (National Skills Development Programme) inayolenga kujenga
ujuzi kwa vijana katika sekta za kilimo, viwanda, teknolojia, nishatina huduma.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa vyuo
vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi, na vijana wa Tanzania kote nchini,
kushirikiana katika kutekeleza kwa vitendo malengo ya Dira ya Taifa 2050.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa
wito kwa Taasisi za biashara, viwanda, na mashirika binafsi kwa kushirikiana na
taasisi za Serikali kuanzisha programu za mafunzo kwa vitendo maeneo ya kazi
ili kukuza stadi za kazi.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia Profesa Daniel Mushi amesema kuwa Wizara inatambua mchango wa
Sekta binafsi katika kukuza nguvu kazi ya Taifa kwa kutoa Elimu kupitia miradi
mbalimbali inayotekelezwa ikiwemo ujenzi wa miundombinu, programu za mafunzo ya
vitendo na utafiti pamoja na kuboresha taasisi binafsi za elimu.
“Pia Serikali imeendelea kuongeza fedha kwa ajili ya
kuboresha mifumo wa upangaji wa utoaji mikopo ya Elimu ya juu kupitia Bodi ya
Mikopo ili kuhakikisha kila mwanafunzi anayetoka katika familia isiyo na uwezo
anapata fursa sawa ya kujifunza.”
Naye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere Prof.
Alexander Makulilo amesema kuwa lengo la kongamano hilo kukuza na kuenzi urithi
wa mwalimu nyerere katika maendeleo ya Rasilimali watu, kubaini njia za
kimkakati za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi inayoweza kuendana na mahitaji ya
Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na kukuza majadiliano baina ya wadau kuhusu sera
na ubunifu.

0 Maoni