Wananchi
wa wilaya ya Bunda mkoani Mara wamekiri kuiona dhamira ya dhati ya Serikali
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA ya kutatua
migongano baina ya wanyamapori na binadamu Kwa kuongeza Idadi ya vizimba, hatua
inayotajwa kupunguza athari Kwa wananchi hao.
Kauli
hiyo imetolewa Oktoba 22, 2025 wakati wa ziara ya kukagua vizimba hivyo ikienda
sambamba na utoaji elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na
wanyampori aina ya mamba na viboko iliyofanywa na maofisa wa TAWA mkoani humo.
Miongoni
mwa wananchi aliyewahi kujeruhiwa na mamba, Kurwa Ryoba mkazi wa Kijiji cha
Buzimbwe ameishukuru Serikali Kwa hatua
hiyo ya kuongeza Idadi ya vizimba akisema vizimba hivyo ni suluhisho muhimu
katika kuokoa maisha ya wananchi, huku akiwasisitiza wananchi wenzake
kutopuuzia kutumia vizimba hivyo ili wasije wakapata madhara aliyoyapata yeye
"Naishukuru
sana Serikali kutujengea kizimba hiki, maana kabla hakijajengwa watu walipata madhara akiwemo ndugu yangu"
alisema Ryoba.
"Wananchi
wenzangu, kizimba hiki kimejengwa hapa lakini naona wengine wanadharau
kukitumia, wakipata madhara wanaanza kuilaumu Serikali. Mimi nawashauri
wajifunze kutoka kwangu, wachukue tahadhali watumie vizimba, Serikali imefanya
maneno mazuri kutujengea vizimba"
ameongeza mkazi huyo wa Kijiji cha Buzimbwe.
Afisa
Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema Kufuatia
changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini hususani katika
mikoa ya Kanda ya Ziwa, Serikali kupitia TAWA katika bajeti ya Mwaka 2024/25 ilitenga zaidi ya
shillingi million 210 Kwa ajili ya kuongeza Idadi ya vizimba vipya Saba (7)
ambapo Kwa wilaya ya Bunda pekee vizimba vinne tayari vimekamilika na
vinaendelea kutumiwa na wananchi.
Aidha
ametoa rai Kwa wananchi hao kuwa na matumizi sahihi ya vizimba hivyo, ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha wanavilinda ili viendelee kuwa msaada kwao.
"Hatujisikii
furaha kusikia wananchi wanapata madhara ya wanyamapori hawa, hivyo ni muhimu
mzingatie matumizi sahihi ya vizimba hivi Kwa ajili ya usalama zaidi ili
kujiepusha athari hizo. Vilevile Serikali imetumia gharama kubwa kuvijenga,
hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuvilinda ili viendelee kuwa msaada,"
alisema Maganja.
Naye
Afisa Uhifadhi Kutoka Kanda ya Ziwa, Sato Masinde amewashauri viongozi wa
vijiji kuunda Sheria ndogo ndogo ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha
miundombinu hiyo inalindwa ipasavyo na kuendelea
kuwanufaisha wananchi hao.



0 Maoni