SAUTI za kampeni za
uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani nchini Tanzania zimechanganyikana na
mvumo wa ajabu unaotoka katika mitandao ya kijamii, ukiongozwa na mwanamke
anayeishi nchi za mbali.
Huyu si mwingine bali
Mange Kimambi, Mtanzania anayeishi nchini Marekani, ambaye kwa muda mrefu
biashara yake imejengwa katika kuuza maudhui yenye kejeli, dharau, na matusi
dhidi ya watu maarufu, wasanii, na sasa, wanasiasa.
Mageuzi ya ajenda ya
Mange yamefikia kilele chake wakati alipoamua kuelekeza mashambulizi yake ya
maneno moja kwa moja kwa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kinachotia shaka
zaidi katika dhamira yake dhaifu ni ile hali yay eye kufikia hatua ya kuanza
kuhamasisha vijana kuandamana kwa nia ya kuitaka Serikali iondolewe madarakani
kwa nguvu, na hata kutoa kauli zenye lengo la kukivuruga Jeshi la Ulinzi kumtii
yeye badala ya utaratibu uliowekwa na Katiba ya nchi.
Hili si jambo dogo, ni mkondo wa hatari
unaopaswa kuzingatiwa na kila Mtanzania anayethamini amani.
Biashara ya Mdomo
Inayokula Bilioni
Kinachoshangaza zaidi
ni ukweli kwamba uchochezi huu umefanywa kuwa biashara yenye faida kubwa.
Inakadiriwa kuwa biashara hii ya uchochezi inamuingizia Mange Kimambi zaidi ya
Shilingi Bilioni 1.5 kila mwezi.
Utajiri huu unatokana
na wafuasi wake zaidi ya milioni moja wanaolipa kiasi cha Shilingi 1,500 kwa
mwezi ili kupata fursa ya kusoma maudhui yake yanayolenga kudhalilisha.
Mbali na michango ya
moja kwa moja kutoka kwa wafuasi, Mange ananufaika na wadhamini na wafadhili
ambao wanapata faida kutokana na chuki, dharau, na kejeli anazotoa dhidi ya
Serikali ya Tanzania.
Hii ni biashara ya
hatari ambayo inalisha chuki ndani ya jamii na kugharimu heshima ya taifa kwa
maslahi binafsi.
Wito kwa Vijana:
Amani ni Jasho, Sio Kelele
Ni muhimu kwa
Watanzania, hasa vijana wanaomfuatilia Mange Kimambi, kuelewa ukweli mmoja wa
msingi: amani haipatikani kwa kelele za matusi au kwa maneno matamu ya
uchochezi; inalindwa kwa vitendo. Amani ya Tanzania imejengwa kwa gharama kubwa
kwa damu na jasho la wazalendo waliojitolea kulinda umoja.
Walinzi halisi wa
amani leo ni vijana wanafanya kazi kwa bidii shambani, viwandani, na ofisini sio
wale wanaotafuta utajiri kwa kuwasha moto wa vurugu kutoka nchi za mbali.
Tanzania bado
haijafika katika hali ya nchi zilizoporomoka kimaadili na kiuchumi kwa sababu
ya fujo na maandamano yasiyo na msingi. Tunayo mifano ya nchi jirani ambako leo
watumishi wa umma hawalipwi mishahara, huduma za afya zimekufa, na wawekezaji
wamekimbia kutokana na machafuko ya kisiasa.
Tanzania bado
inasimama imara, ina utulivu, na ina matumaini makubwa. Tusikubali kamwe
kiongozi anayeishi Marekani kwa zaidi ya miaka 15, asiyeweza hata kukanyaga
ardhi ya Tanzania kutokana na kesi zake za kudhalilisha, atuhubirie namna ya
"kuikomboa nchi" huku yeye mwenyewe hajui hata bei halisi ya unga
huko Kariakoo. Wakati huu wa uchaguzi, busara na utulivu ni ngao yetu kuu.

0 Maoni