Kauli ya "Tanzania si mahali pa majaribio ya
ghasia" imesisitizwa kwa nguvu zote kufuatia barua ya wazi yenye uzito
mkubwa kutoka kwa Profesa Hassan Mahmoud, msomi raia wa Sudan, ambaye kwa sasa
anaishi uhamishoni Dubai kutokana na nchi yake kukumbwa na vita vya wenyewe kwa
wenyewe.
Profesa Mahmoud, ambaye familia yake imepata hifadhi
hapa nchini, anaiita Tanzania "kisiwa cha amani," lakini
anatutahadharisha kuitunza amani hiyo kama "mboni ya jicho."
Profesa Mahmoud anaeleza kwa uchungu na maumivu
jinsi taifa lake, ambalo lilikuwa tajiri na lenye matumaini makubwa,
lilivyoteleza na kuzama katika dimbwi la vita lisilo na mwisho. Katika barua
yake, anasimulia hali ya kutisha aliyoshuhudia ya majirani wakiuana, majiji
yakigeuka magofu, familia zikisambaratika, na mamilioni ya watu wakilazimika
kukimbia makwao yeye akiwa mmoja wao.
Akielekeza ujumbe wake kwa Watanzania, Profesa
Mahmoud anatoa onyo lenye hekima na maumivu: "Kilichotokea Sudan kinaweza
pia kutokea kwenu endapo mtawaruhusu wanaohubiri vurugu kupata nafasi."
Anasisitiza kuwa, migogoro huanza na maneno, maneno
ambayo yanaonekana madogo na yenye kusisimua katika mitandao ya kijamii, lakini
huishia kwa vifo, umaskini, na uharibifu wa miaka mingi ya maendeleo.
Kitisho Kutoka 'Wanaharakati wa Ughaibuni'
Profesa Mahmoud anaitambua Tanzania kama nchi ya
kipekee isiyo na migawanyiko ya kikabila, kidini, wala kiitikadi, na amani ya
miongo mingi haipaswi kuchukuliwa kirahisi. Anahimiza kila Mtanzania kukataa
kwa nguvu zote wale wanaotumia majukwaa ya siasa au mitandao ya kijamii
kuhubiri chuki, fitina, na vurugu.
Jambo jingine la kutia wasiwasi ni kufichua kwake
kuwa ana taarifa za kuaminika kwamba baadhi ya Watanzania walioko nje ya nchi
"wanalipwa ili kutumia mitandao ya kijamii kueneza chuki na kuhamasisha
migawanyiko ya kisiasa."
Msomi huyo ameonya kuwa yuko tayari kuwataja
hadharani wale wote wanaonufaika na fedha hizo za uchochezi endapo wataendelea
kuhatarisha amani ya nchi.
"Hawa 'wanaharakati wa ughaibuni' hawashambulii
viongozi kwa mapenzi ya taifa, bali kwa maslahi yao binafsi," anasema,
akitolea mfano wa maumivu yake ambapo familia yake ilikuwa miongoni mwa
wachache walioweza kutoroka Sudan huku mamilioni wakiendelea kuteseka.
Si Siasa kwa Gharama ya Amani
Ni kweli kwamba kila taifa lina changamoto zake na
Watanzania wanaweza kutamani haki, uwajibikaji, na uongozi bora. Hata hivyo,
haya yote hayawezi kutafutwa kwa gharama ya amani.
Maneno ya Profesa Mahmoud yanatufanya tutafakari:
Amani tuliyonayo haipaswi kuwa chombo cha majaribio ya kisiasa. Ni muhimu
Watanzania tusikubali kurubuniwa na kelele za nje zisizoona machozi ya watoto
wa Sudan au vilio vya kina mama waliosalia bila waume wao kwa sababu ya vita
vilivyochochewa na maneno ya uchochezi kama yanayoenezwa sasa nchini Tanzania.
Huu ni wakati wa kutafakari kwa kina. Ni wajibu wa
kila Mtanzania kulinda misingi ya amani, kutunza urithi wetu wa utulivu, na
kukataa siasa za vurugu na chuki. Tuchukue somo kutoka Sudan, tusisubiri kuona
moshi kabla ya kugundua thamani ya utulivu tulionao leo. Tanzania inahitaji
utulivu wake kuendeleza maendeleo, si majaribio ya ghasia za kisiasa.

0 Maoni