Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw.
Rodney Thadeus, ametoa pongezi za dhati kwa vyombo vya habari nchini kwa
kutimiza wajibu wao wa kuelimisha umma kwa ufanisi mkubwa tangu kuanza kwa
kampeni za Uchaguzi Mkuu hadi sasa.
Bw. Thadeus aliyasema hayo alipokuwa akihojiwa na
mojawapo ya televisheni nchini, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vimekuwa
nguzo muhimu katika mchakato wa uchaguzi.
"Tumeridhishwa na jinsi vyombo vya habari
vilivyochambua habari na kuwalisha wananchi taarifa muhimu kuhusu ilani za
vyama, na nini kinastahili kufanyika siku ya kupiga kura,na baadaye "
alisema Bw. Rodney.
Alieleza kuwa, mafanikio hayo yamechangiwa sana na
vyombo vya habari kufuata Mwongozo kwa Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari
katika Kuripoti Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025. Pia,
alitaja umuhimu wa mafunzo ambayo yaliendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali, yaliyosaidia kuwajengea uwezo waandishi.
Aliongeza kuwa, vyombo vya habari pia vimefanya kazi
nzuri ya kuhimiza amani na kuwatanabaisha wananchi umuhimu wa kupiga kura kama
haki yao ya kikatiba.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi huyo alieleza wasiwasi
wake kuhusu baadhi ya vyama vya siasa ambavyo bado havijatoa ilani zao za
uchaguzi kwa umma, jambo linaloweza kuwanyima wananchi fursa ya kufanya maamuzi
sahihi.
"Ni changamoto kuona kuna vyama bado, mpaka
tunapohojiwa, havijatoa ilani zao. Ilani ndiyo dira na ahadi ya chama kwa
wananchi," Bw. Rodney alieleza.
Bw. Rodney ametoa wito kwa vyama hivyo kutumia siku
chache zilizobaki za kampeni kuelimisha wananchi waziwazi kuhusu nini hasa
wanataka kuwafanyia, badala ya kujikita kwenye siasa za kawaida.
"Tunaviomba vitumie siku hizi chache zilizobaki
kuelimisha wananchi nini hasa wanataka kuwafanyia. Wananchi wanahitaji kujua
mipango ya kina kabla ya kufanya uamuzi wao wa mwisho," alihitimisha.
Kauli hii ya MAELEZO inasisitiza umuhimu wa uwazi na
uwajibikaji wa vyama vya siasa katika kuweka bayana ahadi zao kwa wapiga kura,
huku ikipongeza jukumu muhimu linalotekelezwa na vyombo
vya habari nchini.

0 Maoni