Mradi wa Heet wawezesha ajira za moja kwa moja kwa asilimia 82 ya wahitimu UDSM

 

Asilimia 82 ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wanaingia kwenye ajira moja kwa moja baada ya kuanzishwa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) mwaka 2021.

Kauli hiyo imetolewa jana na Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. Wiilliam Anangisye katika semina ya siku moja na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya mradi huo.

“Miongoni mwa mafanikio ya HEET ni kwamba, haupiti mwaka mmoja zaidi ya asilimia 82 ya wahitimu wanaingia kwenye ajira,” amesema.

Amesema, mradi huo umewezesha wanafunzi wa chuo hicho kuhitimu wakiwa wameiva kwa ujuzi jambo ambalo ndio hitajio kubwa la soko la ajira kwa sasa.

Naibu Mratibu wa HEET, Prof. Liberato Haule amesema, mradi huo umefanikisha kujenga jumla ya majengo 21 katika Mikoa ya Lindi, Kagera, Dar es Salaam na visiwani Zanzibar ili wanaohitaji chuo hicho, waweze kusoma wakiwa katika maeneo hayo.

“Ujenzi wa miundombinu hii umefika asilimia 65. Mradi huu (HEET) kwa ujumla umetekelezwa kwa asilimia 80,” amesema.

Baada ya ziara fupi kwenye baadhi ya majengo mapya ya Mradi wa HEET, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema, UDSM imeondokana na unyumbani kwa kutanua elimu kwenye mikoa iliyojenga majengo yake.

“Hili ni jambo zuri sana, tusimame na mazuri yanayofanywa na nchi, tusipofanya sisi hakuna ambaye atakuja kutusemea,” amesema.

Mradi wa HEET unaotekelezwa kwa miaka mitano (2021 - 2026), umelenga kuimarisha elimu ya juu nchini kwa kuwekeza miundombinu, kuboresha mitaala na kuimarisha ushirikiano kati ya Vyuo Vikuu na Sekta Binafsi ambapo kiasi cha Dola za Marekani Milioni 47.5 zilitengwa kwa ajili ya mradi huo.

Mpaka sasa jumla ya mitaala 250 tayari imeithinishwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

0 Maoni