Mzee
Benson Gabriel Mwakilembe (Maarufu Tall) mchimbaji wa miaka mingi na mmiliki
mwenza wa Kiwanda cha Kwanza cha Kisasa cha kuchenjua shaba nchini cha Mineral
Access Systems Tanzania Ltd (MAST), amesimulia safari yake kutoka kuchimba dhahabu
hadi kuwekeza kwenye shaba. Akizungumza na Madini Diary hivi karibuni, ameeleza
safari yake ya mafanikio, fursa, changamoto na maono kuhusu mustakabali wa
Sekta ya Madini nchini, akisisitiza nafasi ya teknolojia na uwekezaji wa ndani
katika kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.
"Mimi
kwenye dhahabu sirudi tena – sasa niko kwenye shaba. Tanzania tuna shaba nyingi
kushinda hata nchi ya Zambia! Serikali na wachimbaji waione kama zao kuu la
biashara, masoko yapo,’’ anasema Mzee
Mwakilembe.
Akizindua
kiwand hicho Juni 18, 2025 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Kassim Majaliwa alisema kimeiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia kama
mzalishaji wa shaba na hivyo kutimiza dhamira ya Serikali kuongeza thamani ya
madini kabla ya kusafirishwa nje. Alisema ujenzi wa kiwanda hicho unaonesha
dhamira ya Serikali kuongeza thamani ya madini, na uwekezaji wa MAST ni
uthibitisho wa mazingira bora ya biashara nchini.
Kwa
muktadha huo, katika simulizi yake Mzee Mwakilembe anasema, “katazo la kusafirisha
shaba ghafi nje lililotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano tuliona limetuumiza
sana kibiashara, lakini, ndilo limetufikisha hapa. Awamu ya Sita imeweka mkazo
zaidi na sasa ni ajabu, kwa mara ya kwanza, Tanzania tunachenjua shaba hapa na
tumeweza kusafirisha copper cement zaidi ya tani 200,’’ anasema Mzee
Mwakilembe.
Mbali na
leseni za shaba Chunya, Mzee Mwakilembe
pia anamiliki leseni Simanjiro, Tunduru, Mpwapwa na Njombe anazolenga
kuchimba shaba na kusafirishwa Chunya kwenye kiwanda cha MAST na kueleza
kwamba, mpango wa siku za usoni wa kiwanda hicho ni kuchenjua shaba kufikia
kiwango cha copper cathode. ( zao la mwisho).
"Madini
yamenifaa sana – ninaendesha maisha, nina miradi mingine, sasa nina mabasi
mawili ya usafirishaji wa abiria kutoka Tunduru mpaka Mbeya. Nilipotoka na
nilipo sasa ni tofauti kabisa… kwa utani anasema, sasa hivi napanda ndege bana,
– madini yamenivusha, mimi sikubahatika kusoma!” anasema Mzee Mwakilembe.
Hakuacha kupongeza kuhusu namna viongozi wa
Wizara walivyomshika mkono kufika hapo na kusema,’’ kiwanda hiki ni matokeo ya
msaada mkubwa kutoka kwa viongozi wa Wizara. Alianza Mhe. Biteko huyu
alinifundisha namna ya kupambana na wawekezaji, akaja Waziri Mavunde, kiwanda
cha MAST ni nguvu ya Mavunde! Katibu Mkuu Samamba na kijana wangu Rama wa Tume
ya Madini, wametupambania sana, na hapa Chunya huyu Afisa Madini na wenzake,
wana msaada sana. Natamani uongozi huu uendelee," anasisitiza Mzee
Mwakilembe.
Akizungumza
siku ya uzinduzi, Mkurugenzi wa MAST,
Godfrey Kente alisema lengo la kiwanda ni kuchenjua shaba yenye kiwango cha
chini asilimia 0.5 hadi 2 na kuiongeza thamani hadi asilimia 75 kupitia teknolojia ya leaching na
cementation.
Kente
alisema MAST inatarajia kujenga viwanda vitatu vya shaba Manyara, Ruvuma na
Dodoma, ambapo kila kimoja kitatengeneza ajira zaidi ya 500 na kuchangia zaidi
ya Dola za Marekani milioni 40 kwa mwaka katika uchumi.
Akizungumza
hivi karibuni na Madini Diary, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Chunya
Mhandisi Laurent Mayala alisema tangu kuanzishwa kwake Aprili 2025, kimezalisha
tani 810 za shaba zenye thamani ya Sh10.3 bilioni, na Sh 594 milioni tayari
zimetolewa Serikalini.
Kuhusu
MAST
MAST ni
Kampuni ya Kitanzania, iliyoanzishwa mwaka 2011. Kiwanda hicho ni matokeo ya
uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 10 za Kimarekani (USD) ikiwa ni uwekezaji wa
ubia kati ya Kampuni ya MAST na MCC kutoka New York, Marekani.
Ombi kwa
Serikali na taasisi za fedha
"Serikali
kupitia STAMICO ikae na taasisi za fedha – wachimbaji wakopeshwe kwa leseni
zenye tafiti. Pia, wananchi waelimishwe kuhusu sekta ya madini. Mama ametuletea
mashine, lakini ziwafikie wachimbaji wadogo zaidi na gharama za utafiti
zipunguzwe," anasisitiza Mzee
Mwakilembe.
Vipi
kuhusu mageuzi ya Chunya?
"Watu
waliokuwa Chunya miaka ya 1980 wakirudi leo watashangaa sana – Chunya
imebadilika sana! Haikuwa hivi. Serikali imerahisisha sana shughuli za
uchimbaji na biashara ya dhahabu," anasema Mzee Mwakilembe.
Vison
2030: Madini ni Maisha na utajiri



0 Maoni