Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde (MB),
amezindua rasmi shughuli za ujenzi wa mgodi wa madini ya graphite wa Kinywe,
unaotekelezwa na kampuni ya Faru Graphite Corporation kwa ubia kati ya Serikali
ya Tanzania (hisa 16%) na Black Rock Mining Limited (hisa 84%) ikiwa ni hatua
kubwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya sekta ya madini nchini.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika leo tarehe 9
Oktoba 2025 katika eneo la Mahenge, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro, Mhe.
Mavunde amesema uzinduzi huo ni ishara ya kasi mpya ya uendelezaji wa miradi
mikubwa ya kimkakati katika Sekta ya Madini, kutokana na maelekezo ya Mhe. Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mradi huu si uchimbaji wa rasilimali pekee, bali ni
injini ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa viwanda, biashara, ajira, na
ustawi wa jamii katika eneo la Mahenge kwa ujumla,” amesema Waziri Mavunde.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mradi wa Mahenge
unatarajiwa kugharimu takribani dola za Marekani milioni 510,(zaidi ya tsh
trilioni 1.3)na utazalisha ajira zaidi ya 400 wakati wa ujenzi na zaidi ya 900
ajira za kudumu mgodi utakapoanza uzalishaji kamili. Nje ya mgodi, takribani
ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 4,500 zitachochewa kupitia mnyororo wa
thamani wa wachuuzi, wakulima, wasambazaji wa bidhaa na watoa huduma.
Aidha, amesisitiza kuwa, Serikali inatarajia kupata
mapato ya zaidi ya dola bilioni 3.2 (zaidi ya tsh trilioni 7) katika kipindi
cha uhai wa mgodi, kupitia kodi, tozo, gawio, na mrabaha wa madini.
Akifafanua umuhimu wa madini ya graphite, Waziri
Mavunde amesema madini hayo ni miongoni mwa madini muhimu katika utengenezaji
wa betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki, na paneli za umeme wa jua
na kuwa kupitia mradi huo na mengine iliyopo nchhui Tanzania inajiweka kama
kitovu cha malighafi za teknolojia safi duniani.
Pia, Waziri Mavunde ameitaka Kampuni ya Faru
Graphite Corporation kuzingatia matakwa ya
Ushikishwaji wa Watanzania (local content) na Uwajibikaji kwa Jamii
(CSR) kwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania, hususan wananchi wa vijiji
vinavyozunguka mgodi, na kutoa fursa kwa makampuni ya ndani kushiriki katika
mnyororo wa ugavi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Mhe. Adam Malima, amemshukuru Waziri Mavunde kwa uongozi na usimamizi
wake thabiti katika Sekta Madini, akibainisha kuwa Mkoa wa Morogoro umebahatika
kuwa mwenyeji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo huu wa Faru Graphite wenye
thamani ya takribani Shilingi Trilioni 1.3.
“Huu ndio mradi mkubwa zaidi kuwahi kutekelezwa
katika Mkoa wa Morogoro,” amesema Mhe. Malima, huku akielekeza wataalamu wa
mkoa kuandaa semina maalum zitakazowaelimisha wananchi kuhusu fursa za kiuchumi
na kijamii zitakazotokana na mradi huo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga alisema Serikali ilitoa
leseni ya uchimbaji mkubwa mwaka 2024, na tayari fidia ya zaidi ya Shilingi
Bilioni 13 imelipwa kwa wananchi 254 waliopisha eneo la mradi, ambao pia
watajengewa nyumba mpya.
Ameongeza kuwa miundombinu ya umeme wa kilovolt 220
kutoka Mahenge imeanza kuandaliwa ili kuhakikisha mgodi unapata umeme wa
uhakika, sambamba na kuanzishwa kwa miradi ya kijamii (CSR) inayolenga elimu,
afya na maji.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Ndg. Nehemiah
Mchechu, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Faru Graphite Corporation, amesema
Serikali kupitia ubia huu inalinda maslahi ya taifa, ikinufaika kupitia hisa,
kodi, ajira na mzunguko wa fedha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi na Mwakilishi wa
Bodi ya Wakurugenzi wa Faru na Blackrock Mining, Black Rock Mining Limited,
Ndg. Richard Crookes, amesema kampuni yake imejipanga kuhakikisha utekelezaji
wa mradi unafuata viwango vya kimataifa vya usalama na uhifadhi wa mazingira,
sambamba na kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira na pia wamemshukuru
Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi yaliyopokea uwekezaji
huo mkubwa Morogoro.



0 Maoni