Wananchi wa kata za Endulen, Alaetoli na Kakesio
zilizopo eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji
unaotekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambapo kwa kata ya Endulen
kisima chenye urefu wa mita 250 chenye
uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita za maji 80,000 kwa siku kimechimbwa katika
eneo la Mlima Matiti kata ya Endulen.
Akiwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa mradi huo
ambao utekelezaji wake upo zaidi ya 50%, Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Abdul-Razaq
Badru ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia wananchi wa kata za
Endulen, Alaetoli, Kakesio na baadae Olbalbal ili kukabiliana na changamoto ya
upungufu wa maji kwa mifugo hasa msimu wa kiangazi.
“Hapa kata ya Endulen baada utafiti tumepata maji ya
kutosha, kisima kilichochimbwa katika eneo hili kitazalisha lita 8,000 kwa saa
na lita laki moja (100,000) kwa siku, tunaamini ndani ya wiki moja majaribio ya
mwisho ya kujaza maji yatakuwa yamekamilika, mabwawa ya kukusanya maji
yatachimbwa na mifugo zaidi ya 2000 itakuwa inapata maji hapa kila siku,”
alifafanua Badru.
Kamishna Badru ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi
hiyo kwa ajili ya wananchi wanaoishi eneo la hifadhi ya Ngorongoro ni sehemu ya
utekelezaji wa miradi ya kijamii ambayo wananchi waliomba Mamlaka hiyo
kuwasaidia ili kukabiliana na changamoto za ukame na kuepuka kuingiza mifugo
maeneo maalum ambayo hayaruhusiwi kuingiza mifugo ndani ya hifadhi.
Baada ya kukamilika mradi wa maji kata ya Endulen,
visima vingine vitachimbwa katika kata za Kakesio na Olbalbal ambapo wananchi
watanufaika kwa kunweshea mifugo yao pamoja na matumizi ya Nyumba.
Mmoja wa wananchi wa Kata ya Endulen Siyapaa
Ole-Keyan amesema utekelezaji wa miradi katika kata hizo Serikali imejibu kilio
cha kunusuru mifugo yao hasa kipindi cha kiangazi na wao kujiepusha kupeleka
mifugo yao maeneo yasiyoruhusiwa katika nyanda za misitu na eneo la Ndutu
ambalo ni mazalia ya Nyumbu wanaohama.




0 Maoni