Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi
Rogatus Mativila, amemtaka Mkandarasi JUIN Company Ltd anayekarabati barabara
ya Nyamwage-Tawi-Kikobo yenye urefu wa Kilomita 56 kwa kiwango cha changarawe
wilayani Rufiji mkoani Pwani, kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili
kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Mhandisi
Mativila ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa barabara
hiyo ya Nyamwage-Tawi-Kikobo ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 35.
"Mradi
huu umechelewa na mvua zinakuja, kwa hali ilivyo mvua zikianza kunyesha kazi
zitakuwa hazifanyiki, ninachosisitiza kabla mvua hazijanyesha Mkandarasi afanye
kazi usiku na mchana ili kazi ikamilike kwa wakati, pia naomba TARURA msimamie
kwa ukaribu ili barabara hii iweze kupitika,” amesema.
Aidha,
Mhandisi Mativila amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza fedha
za bajeti ya TARURA kutoka Shilingi Bilioni 275 hadi Shilingi Bilioni 700 kwa
ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara za wilaya ili ziweze kusaidia
shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kwa
upande wake, Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahim Kibasa amesema
wamejipanga kuhakikisha utekelezaji wa kazi zote zinazoendelea za mwaka wa
fedha 2024/25 utekelezaji wake unakamilika ambapo ametoa wito kwa Makandarasi
wote wanaotekeleza kazi za TARURA mkoa wa Pwani hasa wale ambao wamekuwa
wakichelewesha kazi warudi “site” ili kukamilisha kazi hizo.
“Tunawaomba
Makandarasi kufanya kazi kama mikataba inavyowataka kwasababu vinginevyo
tunaweza kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yao, hatuwezi kuvumilia kazi
zimekuwa hazifanyiki kwa wakati, sisi tutakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha
tunasimamia kwa ukaribu kazi hizo kama Naibu Katibu Mkuu alivyotuelekeza,” amesema.
Akitoa
taarifa ya mradi, Meneja wa TARURA wilaya ya Rufiji, Mhandisi Nicholaus
Ludigery amesema kuwa mradi huo upo katika awamu mbili ambapo ni ukarabati wa
barabara ya Nyamwage-Tawi Km 28 kwa kiwango cha changarawe kwa thamani ya
Shilingi 1,163,543,000 utekelezaji umefikia asilimia 35 pamoja na ukarabati wa
barabara ya Nyamwage-Tawi-Kikobo kwa thamani ya shilingi 998,780,000
utekelezaji umefikia asilimia 5.
Ameongeza
kuwa kukamilika kwa barabara hiyo itasaidia kuzifikia huduma za kijamii kama
elimu na afya na pia kuchochea shughuli za kiuchumi kama biashara na kilimo
kwani wananchi wa maeneo hayo wanajishughulisha na kilimo cha korosho, ufuta,
machungwa, mihogo na minazi ambapo barabara hiyo itawasaidia kukuza pato la
mwananchi mmoja mmoja na wilaya ya Rufiji kwa ujumla.


0 Maoni